Kila la Kheri Simba, Endeleeni Kutetea Heshima ya Tanzania
WIKIENDI ya ngumu kwenye soka la Tanzania inaendelea. Timu zetu nne zinazotuwakilisha kwenye michuano ya kimataifa zinaendelea kupambana kwa masilahi ya Taifa. Tayari KMC, Azam na Yanga zimeshajitupa Uwanjani juzi na Jana.
Leo ni siku ya Mabingwa wanchi, Simba SC ambayo itakuwa kwenye Uwanja wa Taifa kurudiana na UD Songo ya Msumbiji. Simba katika mchezo huo inahitaji ushindi wowote kusonga mbele kutokana na matokeo ya awali ambayo yalikuwa ni suluhu.
Ndio mchezo wa kwanza wa Simba kimataifa msimu huu akiwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani. Twende tukawasapoti. Kuna kila sababu Watanzania wote kuwa nyuma ya Simba kwa kila hali ndani na nje ya Uwanja kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri kwenye mchezo huo muhimu.
Kama tulivyotoa sapoti kwa timu zingine na leo tumiminike kwa wingi jioni ndani ya Uwanja wa Taifa kuisapoti Simba ambayo inaonekana imejiandaa kisaikolojia kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.
Kila shabiki anakumbuka nguvu kubwa na mbinu walizotumia msimu uliopita na kufanikiwa kwenye mashindano hayo hadi kufikia hatua ya robo fainali. Mafanikio ya Simba msimu uliopita ndiyo yameipa Tanzania heshima ya kuongezewa timu nne kwenye michuano ya Afrika.
Itakumbukwa kwamba msimu huu kimataifa, Tanzania iliwakilishwa na Simba, Yanga, Azam na KMC. Ni jambo ambalo halikuwahi kutokea katika misimu ya hivi karibuni kwa nchi za Afrika Mashariki kutokana na ufanisi mbovu wa timu za nchi hizo kwenye mashidano hayo makubwa Afrika.
Upendeleo waliopewa Tanzania na CAF umezishtua nchi nyingine ambazo zimelazimika kuongeza juhudi na kuwekeza kwenye soka.
Heshima yote hiyo imetokana na juhudi za Simba kwenye mashindano hayo makubwa ndio maana tunatoa rai kwa mashabiki kumiminika kwa wingi leo kwenye Uwanja wa Taifa kuipa nguvu Simba na kuilipa fadhila kutokana na ushujaa wao wa msimu uliopita.
Simba ina uwezo wa kufanya vizuri kwa vile imefanya usajili mzuri na imekuwa na muda mrefu wa maandalizi ndani na nje ya nchi.
Inapofika kwenye mambo ya kimataifa kama hili la leo tunasisitiza Watanzania wote kuwa rangi moja kwa heshima ya soka la nchi. Kufanya vizuri kwa klabu zetu kimataifa kuna masilahi mengi ikiwemo kukuza soka la klabu husika, nchi pamoja na kuongeza soko la wachezaji wetu nje ya mipaka ya Afrika.
Soka letu lilikuwa limekwama kwa miaka mingi sasa kwa vile tumeanza kupata mwanga tupambane kwa pamoja, tuwahimize na kuwapa moyo wawekezaji wetu ili wazidi kuwekeza na kukuza soka letu kwa vile soka linahitaji fedha kwenye mambo mbalimbali.
Wawekezaji kama Mohammed Dewji ‘Mo’ wanahitaji kupewa moyo kwa kujazana Uwanjani siku muhimu kama ya leo ili kusapoti kile wanachofanya pamoja na maendeleo ya timu kwa ujumla.
Ni matumaini yetu hata wachezaji watajituma kwa nguvu wakikumbuka na kuzidisha juhudi za msimu uliopita ambazo ziliwajengea heshima na kuwapa muda muda wa kusafiri na kujifunza mengi yanayoendelea Duniani. Tukutane Taifa kuipa sapoti Simba, Simba moja, Tanzania moja. Tuweke masilahi nchi mbele.
MAGOLI YA AZAM FC VS FASIL KENEMA 3 -1
The post Kila la Kheri Simba, Endeleeni Kutetea Heshima ya Tanzania appeared first on Global Publishers.
No comments: