KAMPUNI YA MAFUTA YA PUMA YAPELEKA ELIMU YA USALAMA BARABARANI KWA WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI ZANZIBAR
Na Mwandishi Wetu,Zanzibar
NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amesema kuna kila sababu ya kuendelea kutolewa elimu ya usalama barabarani na matumizi sahihi ya barabara zetu ili kupunguza ajali zinazosababisha ulemavu na vifo kwa watu wasio na hatia nchini.
Pia amesema kwa sasa Wizara hiyo ipo kwenye mchakato wa kuangalia upya sheria za usalama barabarani kwa lengo la kuziongezea ukali sheria hizo ili kukabiliana na watumiaji wa vyombo vya moto na hasa bodaboda ambao wengi wao wamekuwa wakivunja sheria mara kwa mara na kusababisha ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Mhandisi Masauni ameyasema hayo wakati wa utoaji zawadi kwa wanafunzi na shule za msingi ambazo zimeshinda michoro yenye ujumbe wa usalama barabarani visiwani humo kwa mwaka 2019, ambapo Shule ya Msingi Mkunazini imepata kitita cha Sh.milioni nne kutoka kwa Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania baada ya kuibuka mshindi wa kwanza.
Mafunzo hayo ya elimu ya usalama barabarani yamefadhiliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma Tanzania ndio mara ya kwanza kutolewa visiwani humo.
"Kuna umuhimu mkubwa wa jamii yetu ya Watanzania kwa upande wa Bara na Visiwani kuendelea kupatiwa elimu inayohusu uslama barabarani pamoja na matumizi sahihi ya barabara zetu.
"Hivyo nitumie nafasi hii kuipongeza Kampuni ya Puma Tanzania kwa uamuzi wake wa kutoa elimu hii ambapo kwa hapa Zanzibar shule tano za msingi zimepata elimu hiyo na tunaamini itasaidia kupunguza ajali ambazo zinaweza kuepukika,"amesema Mhandisi Masauni.
Ameongeza kuwa kutolewa kwa elimu ya usalama barabarani kwa wafunzi kutasaidia kuokoa maisha yao na kuwapusha na ajali kwani watakuwa na uelewa mzuri wa kutumia barabara zetu.
Ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mikakati ya Serikali katika kuendelea kukabiliana na ajali za barabarani nchini na moja ya mkakati ni pamoja na kusimamia sheria zilizopo na kuongeza wanaendelea na mchakato wa kupitia upya sheria za usalama barabarani ili ziwe kali zaidi.
"Ajali za barabarani zimeendelea kupungua siku hadi siku, lakini bado kunachangamoto ya baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto na hasa waendesha bodaboda wanavunja sana sheria za barabarani.
"Tumeamua atakeyakamatwa kwa kuvunja sheria za usalama barabarani awekwe mahabusu na kisha apelekwe mahakamani ili sheria ichukua nafasi yake.Wanavunja sheria kwa kuamini sheria sio kali sana, sasa tumeamua na tutawadhibiti ipasavyo kwa watakaoendelea kutoheshimu sheria zilizopo,"amesema.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania Ltd Dominic Dhanan amesema kuwa elimu ya usalama barabarani imetolewa kwa shule tano za msingi za Zanzibar.
"Tumekutana hapa kwa ajili ya kutoa zawadi kwa wanafunzi wa shule za msingi walioshinda shindano la michoro ya Usalama barabarani kwa mwaka 2019 kisiwani Zanzibar.
"Tukio hili la utoaji zawadi linahitismisha prgramu iliofanywa na kampuni ya Puma kwa ushirikiano na Shirika lisilo la kiserikali la AMEND kupitia New vision Consortium trainers ya Zanzibar wa kutoa elimu ya usalama barabarani,"amesema.
Amefafanua programu hiyo ilihusisha mafunzo kuhusu usalama barabarani katika shule za Msingi Mwembeshauri, Kisiwandui, Shule ya Msingi Jang’ombe, Shule ya Msingi Nyerere na Shule ya Msingi Mkunazini.
"Wanafunzi wasiopungua 6500 wamapeta elimu hiyo ambayo imekwenda sambamba na uchoraji wa michoro inayohamasisha matumizi sahihi ya barabarani na kufuata sheria zilizopo,"amesema.
Ameongeza programu hiyo ya usalama barabarani ni mwendelezo wa kampeni ambayo ilizinduliwa rasmi mwaka 2013 ambapo zaidi ya shule 80 zimefikiwa na jumla ya wanafunzi 106,500 wamepata mafunzo katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Ruvuma, Dodoma na sasa visiwani Zanzibar.
Ametumia nafasi hiyo kueleza Kampuni ya Puma ya Tanzania imeamua kufika visiwani Zanzibar kwa sababu ya ukuaji wa shughuli za utalii na za kiajamii ambazo zimesababisha ongezeko la watu na magari ambayo yanahatarisha usalama wa watoto wanapokwenda shule na kurudi nyumbani.
"Lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto hawa kuwa na uelewa wa matumizi ya barabara wakiwa bado wadogo.Kwa kufanya hivyo tunawaongezea uelewa kuhusu dhima nzima ya usalama barabarani kwa waTanzania wengi zaidi,"amesema Dhanah.
Kwa upande wake Mwanafunzi wa shule ya Msingi Mkunazini ambaye ameibuka ushindi wa kwanza kwa mwaka 2019 kwa kuchora mchoro bora wenye ujumbe wa usalama barabarani Raya Zuberi Hemed ambaye amejinyakulia Sh.500,000 ameishuku kampuni ya Puma kwa kutoa elimu hiyo na kuahidi atakuwa balozi wa kueleza matumizi sahihi ya alama za barabarani.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambae pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Usalama Barabarani Nchini, Mhandisi Hamad Masauni (katikati), Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Puma, Dominic Dhanah (watatu kushoto) na Mrajisi wa Jumuiya sisizo za Kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid Abdullah (watatu kulia) wakikabidhi mfano wa Hundi ya Shilingi Milioni Nne kwa Uongozi wa Shule ya Msingi Mkunazini baada ya mwanafunzi Raya Zubeir Hemed(kulia), kuibuka mshindi wa kwanza kwenye Shindano la Uchoraji wa Michoro ya Elimu ya Usalama Barabarani kwenye hafla iliyofanyika Visiwani Zanzibar.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambae pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Usalama Barabarani Nchini, Mhandisi Hamad Masauni, akimpa zawadi mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mkunazini, Saidat Jumbe zawadi baada ya kujibu swali lililohusiana na Kanuni za Uvukaji wa Barabara ili kuepuka ajali.Hafla hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa Shindano la Uchoraji wa Michoro ya Elimu ya Usalama Barabarani iliyofanyika Visiwani Zanzibar.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambae pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Usalama Barabarani Nchini, Mhandisi Hamad Masauni, akimkabidhi kikombe mshindi wa kwanza wa Shindano la Uchoraji wa Michoro ya Elimu ya Usalama Barabarani mwanafunzi wa Shuke ya Msingi Mkunazini Rayah Zubeir Hemed.Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Puma,Dominic Dhanah.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Puma,Dominic Dhanah, akimkabidhi zawadi Mshindi wa Pili Salum Ali Khatib baada ya kushika nafasi hiyo katika Shindano la Uchoraji wa Michoro ya Elimu ya Usalama Barabarani lililodhaminiwa na kampuni hiyo.Hafla hiyo imefanyika Visiwani Zanzibar.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Mrajisi wa Jumuiya sisizo za Kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid Abdullah akimkabidhi zawadi mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kisiwandui,Salma Ali Seif baada ya kujibu swali lililohusiana na usalama barabarani, wakati wa Hafla iliyofanyika Visiwani Zanzibar.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
No comments: