HUU NDIYO UNDANI MAMA ALIYEPATA ‘PANCHA’ ANGANI!
IRINGA: Hii ni kali ya mwaka! Ndivyo unavyoweza kusema juu ya tukio la mama mmoja aliyedaiwa kupata ‘pancha’ angani na kudondokea juu ya paa la nyumba ya mchungaji, Amani lina undani wa tukio hilo. Tukio hilo la aina yake lilijiri Jumapili iliyopita huko Ilula Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa majira ya saa 11:00 alfajiri nyumbani kwa Nabii Jeremia Charles na kuibua gumzo la aina yake.
Habari za awali kutoka kwa mchungaji zilieleza kuwa, alivamiwa na jeshi la washirikina zaidi ya wanne wakitaka kumdhuru. Ilidaiwa kuwa, kutokana na maombi ya mchungaji huyo, mmoja wa wanaodaiwa washirikina hao alidondoka na kunasa juu ya paa huku wenzake wakitoka nduki.
KAMANDA WA POLISI
Kufuatia taharuki hiyo, mapema Jumatatu iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa (RPC), ACP Juma Bwire alisema kuwa, mama huyo aliyepata pancha angani alitambulika kwa jina la Kabula Masunga, mwenye umri wa miaka 41 ambaye ni mkazi wa mkoani Morogoro.
Kamanda Bwire alisema kuwa, mwanamke huyo inadaiwa alikutwa akifanya vitendo vya kishirikina katika mazingira hayo akiwa amejifunga mavazi ya rangi nyekundu na nyeusi huku akiacha kifua chake wazi. “Aidha alikutwa na ungo uliofungwa kitambaa cha rangi nyeusi na nyekundu,” alisema Kamanda Bwire na kuongeza:
“Katika maelezo yake alidai kuwa alikuwa na wenzake wanne ambao walisafiri kwa kutumia ungo wakitokea mkoani Morogoro.” Alisema kuwa, mwanamke huyo alikutwa akiwa na pembe ya ng’ombe na alijifunga hirizi mikononi.
Kamanda Bwire aliongeza kuwa, mwanamke huyo alidai kuwa yeye na wenzake hao wanne walikuwa wakisafiri kwa kutumia ungo. Alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linaendelea kumshikilia mwanamke huyo kwa mahojiano zaidi ili kufahamu lengo la kufanya tukio lake hilo.
MCHUNGAJI
Kwa upande wake Nabii Jeremia alisema kuwa, alikuwa na maombi ya wiki nzima. “Jumapili ndiyo ilikuwa hitimisho la maombi. Kwa hiyo alfajiri ya Jumapili, watumishi wenzangu walinisindikiza kurudi nyumbani kwa ajili ya kujiandaa na ibada. “Nilipofika nyumbani nilimkuta mdogo wangu ambaye aliniambia kuna mambo yametokea hapa. “Nikamuuliza mambo gani? Akasema kulikuwa na kelele usiku, kuna kitu nilikiona.
“Akasema kuna watu aliwaona wakipanda kwenye paa la nyumba na kushuka. Akajua ni wezi waliokuwa wanaiba king’amuzi. “Alipofungua mlango kutoka nje, akamuona mtu akikimbia, akajua ni wezi walitaka kuiba king’amuzi.
“Alipotoka nje akaona mwanaume na mwanamke, akaanza kuwakimbiza ambapo alifanikiwa kumkamata mwanaume. Anasema alipomkamata alishangaa mtu huyo akaponyoka na kutoweka mikononi mwake. “Baada ya mdogo wangu kutusimulia hivyo, tulianza kufanya maombi ndipo tukasikia kishindo nje, tulipotoka ndipo tukabaini kulikuwa na mtu amelala kama maiti kwenye paa ya nyumba yangu.
“Tulipoona hali hiyo ndipo tukapiga simu polisi kuwaambia kuna tukio ambalo hatulielewi hapa nyumbani kwangu, kuna mtu amelala kwenye paa. “Baada ya hapo polisi walifika nyumbani kwangu wakamchukua yule mwanamke.
“Kiukweli mimi hili ni tukio la kwanza kumuona mtu anayedaiwa ni mshirikina. “Katika mahojiano na polisi alisema alikodiwa na washirikina wa hapa Iringa ambao walidai wamezidiwa nguvu. “Mimi ninaamini kama ni nguvu za giza sasa zimeshindwa na ukuu wa Mungu umeonekana.”
The post HUU NDIYO UNDANI MAMA ALIYEPATA ‘PANCHA’ ANGANI! appeared first on Global Publishers.
No comments: