PSPTB YAJIZATITI KUTOA HUDUMA BORA KWA WATEJA KWA KUZINGATIA MISINGI YA UFANISI NA MAADILI
* Washauriwa utumiaji wa dawati la ushauri na maoni kuwa endelevu ili kujenga uadilifu na ufanisi kwa wafanyakazi
KATIKA kuadhimisha wiki ya utumishi kwa Umma bodi ya wataalamu wa manunuzi na ugavi nchini (PSPTB) imeendelea kuadhimisha wiki hiyo kwa kutoa huduma na kusikiliza maoni na kero mbalimbali kutoka kwa wateja wao.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na wateja, Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya wataalumu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi amesema kuwa wiki ya utumishi kwa Umma mwaka huu imeanza tarehe 17 na itafikia kikomo tarehe 23 mwezi huu, na taasisi zote za serikali zimepata nafasi ya kusikiliza changamoto za wateja ikiwa ni pamoja na kutoa huduma kwa ukaribu zaidi.
Amesema kuwa kupitia nafasi yake ya kaimu mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo wameandaa dawati maaalumu ambalo maafisa wa sekta husika za ununuzi na ugavi watakuwepo na baada ya kuhudumiwa watapita katika dawati na kueleza namna walivyohudumiwa na changamoto wanazozipata ili ziweze kutatuliwa.
Amesema kuwa maoni yote yatakayotolewa na wananchi na wateja yatafanyiwa kazi na bodi ya wataalamu ya ununuzi na ugavi na watahakikisha maeneo yote ya ununuzi na ugavi yanafanyiwa kazi kwa umakini na kuhakikisha uaminifu na uadilifu kwa wafanyakazi unazingatiwa.
Kuhusiana na namna huduma zinavyotolewa katika bodi hiyo Mbanyi amesema kuwa; wakati wote wa utoaji huduma wamekuwa na kitengo maalumu cha usiri ambacho wateja hupita mara baada ya kupata huduma na kutoa maoni na kero zao.
Aidha amesema kuwa wamedhamiria na watahakikisha wanafanya kazi kwa manufaa ya taifa na kusema kuwa watashirikiana na wizara washirika katika kuhakikisha azma ya taifa inafanikiwa.
Vilevile amesema kuwa wataalamu wanaosomea fani hiyo ya manunuzi na ugavi wanawatambua kupitia usajili na na kwa kushirikiana na wizara ya fedha na mipango na ofisi ya Rais utumishi katika kuhakikisha suala la ajira kwa wataalamu wa fani hiyo linatekelezwa kwa urahisi.
Kwa upande wake Eliakim Paul ambaye pia ni mteja wa bodi hiyo amesema kuwa dawati hilo la maoni na ushauri lisiwe kwa kipindi cha wiki ya utumishi kwa Umma bali liwe endelevu ili waweze kupokea maoni ya wateja na kuyafanyia kazi kwa wakati.
Na ameeleza kuwa uwepo wa dawati hilo kila siku pia utaongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa wafanyakazi wa bodi hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya wataalumu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi (kushoto) akizungumza na wateja waliofika katika ofisi ya Bodi ya wataalumu wa Manunuzi na Ugavi kwa ajili ya kupewa huduma wakati wa wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza terehe Juni 17 hadi juni 23. Kulia ni Afisa mwandamiza Masoko na mahusiano kwa Umma wa Bodi ya wataalumu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Shamim Ally Mdee.
Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya wataalumu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Godfred Mbanyi akiwaonesha wateja wao namna wanavyofanya kazi katika ofisi hiyo wakati wa wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza terehe Juni 17 hadi Juni 23 mwaka huu.
Afisa mwandamiza Masoko na mahusiano kwa Umma wa Bodi ya wataalamu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Shamim Ally Mdee(katikati) akimsikiliza mteja alipofika kwenye dawati la ushauri na maoni ili kusikiliza kero na changamoto wanazozipata wanapopewa huduma wakati wa wiki ya Utumishi wa Umma. Kulia ni Afisa Mipango ( PSPTB), James Maghori
No comments: