Katibu Mkuu: Kampeni ya marufuku ya mifuko ya plastiki inaenda vizuri
Serikali imesema kampeni ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki inakwenda vizuri na kusisitiza ni makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio vya bidhaa maalumu na kutumika kama mifuko ya kubebea bidhaa mbalimbali huku.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo amebainisha hayo leo jijini Dodoma alipozungumzia azma ya Serikali ya kuendesha operesheni maalumu nchi nzima ya uzingatiaji wa sheria ya usimamizi wa mazingira juu ya marufuku ya mifuko ya plastiki na matumizi endelevu ya mifuko mbadala.
Alisema adhabu stahiki zitatolewa kwa watengenezaji, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa vifungashio vya plastiki vilivyozalishwa ama kuingizwa nchini na kutumika kama vibebeo vya bidhaa.
"Baada ya kuanza kwa utekelezaji wa Katazo la Kutumia mifuko ya Plastiki imebainika kuwa baadhi ya wazalishaji na wasambazaji wamebadilisha matumizi ya mifuko laini ya plastiki isiyokuwa na mishikio na kuitumia kama vibebeo vya bidhaa," alisema Mhandisi Malongo.
Alisema Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na kikosi kazi inaendelea na zoezi la kuelimisha umma juu ya jambo hili pamoja na kuhamasisha matumizi ya mifuko mbadala.
Kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki za Mwaka 2019, ni marufuku kuzalisha, kuingiza nchini, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki iliyotajwa katika Katazo hili.
Alisema Kanuni ya 9 inatoa msamaha kwa baadhi ya vifungashio vya plastiki kwa ajili ya huduma za afya au ambavyo vinatumika kwenye kufungashia bidhaa za viwandani, sekta ya ujenzi, sekta ya kilimo, vyakula au usafi na udhibiti wa taka.
"Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaanda viwango kwa vifungashio hivi ambavyo vitalazimisha kiwango cha unene, uwekwaji lakiri na kutambulisha bidhaa iliyofungashwa kabla ya kuuzwa," alisema.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo (katikati) akifafanua kuhusu vifungashio alipozungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)jijini Dodoma. Wengine pichani kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine na Mkurugenzi Mkuu Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo akionesha baadhi ya viungashio vinavyotumika kwa matumizi ya kubebea bidhaa nyingine tofauti na inayotakiwa.
Naibu Katibu Ofisi ya Makamu wa Rais Balozi Joseph Sokoine akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo akionesha mfuko mbadala unaoruhusiwa kubebea.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo akionesha kifungashio kilichofungwa nyama bila kukidhi vigezo vinavyotwakiwa.
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kufafanua nkuhusu vifungashio.
No comments: