MWAKYEMBE AMTAMBULISHA RASMI KAIMU KATIBU MTENDAJI WA BODI YA FILAMU.
* Dkt. Kiagho Kilonzo ahaidi kuleta mabadiliko na kuhakikisha
Filamu inakuwa jukwaa rasmi la uchumi hapa nchini.
Na.Khadija seif,Globu ya jamii
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe mapema leo amekutana na Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Filamu nchini katika ofisi za Bodi ya Filamu na kumtambulisha kwa Wajumbe wa Bodi hiyo Kaimu Katibu Mtendaji mpya wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo.
Katika kikao hicho Mhe. Mwakyembe alipongeza jitihada chanya zilizoanza kufanywa na Naibu Katibu Mtendaji huyo katika kipindi kifupi cha kuteuliwa kwake na kumtaka kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu katika kuhakikisha Sekta ya Filamu na Michezo ya Kuigiza inasonga mbele na kuwa sehemu ya pato kwa Taifa na Wanatasnia
wenyewe.
“Sekta ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ni moja ya Sekta kubwa na muhimu
zinazoweza kukuza pato la nchi na kupunguza umaskini kwa raia wake, hivyo Bodi ya Filamu ni wajibu wenu kutengeneza mazingira rafiki yatakayo wezesha Sekta hii kukuwa hapa nchini na kupunguza umaskini kwa Watendaji wake” Dkt. Mwakyembe alisema.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji mpya wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo alimshukuru Waziri Mwakyembe kwa kushiriki katika kikao hicho cha kutambulishwa kwake kwa Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Filamu na kumuahidi kuendelea kufanya kazi nzuri itakayoimarisha na kukuza Tasnia ya Filamu kwa kushirikiana na Wajumbe hao wa bodi ya Ushauri inayoongozwa na Mwenyekiti wake Profesa Frowin Nyoni, kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Sekta ya Filamu na kuimarisha umoja wa vyama vya Watendaji katika Filamu ili kuhakikisha
Filamu inakuwa jukwaa rasmi la uchumi hapa nchini.
“kwa pamoja tutashirikiana katika kuifanya Sekta ya Filamu na Michezo ya Kuigiza inakuwa na mchango chanya kwa Taifa letu na sio sehemu au jukwaa la kuharibu maadili ya kitanzania, hivyo tunaahidi kuifanya Sekta hii kuzidi kuimarika ili iweze kuwa jukwaa la moja kwa moja la pato la mtu binafsi na Taifa kwa ujumla”.
Hata hivyo bodi ya Ushauri ya Bodi ya Filamu kwa sasa ina wajumbe 8 ikiongozwa na Mwenyekiti Profesa. Frowin Nyoni na Katibu Dkt. Kiagho Kilonzo ambaye ni Naibu Katibu Mtendaji wa Bodi.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akisisitiza jambo wakati wa Kikao cha kumtambulisha kwa Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Bodi ya Filamu Tanzania Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo (kulia) katika Ukumbi wa mikutano wa Bodi hiyo iliyopo Mtaa wa Samora Posta jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo
Profesa Frowin Nyoni.
No comments: