IGP Sirro Awatoa Hofu Wananchi Tishio la Ugaidi Tanzania
JESHI la Polisi nchini limewatoa hofu wananchi juu ya tishio la ugaidi katika maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam, likisema taarifa hizo zimeshaanza kufanyiwa kazi.
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, ameiambia Mwananchi usiku wa Juni 18, 2019, kuwa jeshi lake lilishapata fununu za shambulio hilo kabla ya Ubalozi wa Marekani nchini kutoa tahadhari juu ya tukio hilo kupitia tovuti yake Juni 18, 2019.
Akizungumzia taarifa hiyo ya ubalozi huo, wa Marekani Sirro amesema, “hiyo ni taarifa kama taarifa nyingine, inaweza kuwa ya kweli au uongo, lakini sisi kama vyombo vya ulinzi huwa hatupuuzi jambo. Tangu jana (Jumanne Juni 17, 2019) tulipata hiyo taarifa kwa hiyo tuko vizuri, timu zetu za operesheni na intelijensia na wengine tunaifanyia kazi.”
Tangazo la ubalozi huo linaeleza kuwapo kwa uvumi wa kutokea kwa shambulio la kigaidi katika eneo la Masaki hususan hoteli za kitalii na maduka ya maeneo hayo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi.
Ubalozi huo umewataka wakazi kuwa makini na maeneo hayo, kujiepusha na makundi na kufuatilia taarifa kupitia vyombo vya habari.
The post IGP Sirro Awatoa Hofu Wananchi Tishio la Ugaidi Tanzania appeared first on Global Publishers.
No comments: