HATARI YA KUHARIBIKA KWA CHUJIO ZA FIGO (GLOMERULONEPHRITIS)
KUHARIBIKA kwa chujio za figo kitaalamu Glomerulonephritis ni aina ya ugonjwa wa figo unaoathiri sehemu maalum ya figo (chujio) inayohusika na uchujaji wa maji pamoja na uchafu kutoka katika damu. Sehemu hii huitwa glomelurus au chujio kama tutakavyokuwa tukitumia katika mada hii.
Mara nyingi chanzo halisi cha kuharibika kwa chujio za figo unaweza kusababishwa na kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili na husababisha damu pamoja na protini kuingia katika mkojo. Tatizo hili hukua kwa haraka na figo linaweza kupoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kwa kasi ndani ya muda mfupi, kitalaamu ni rapidly progressive glomerulonephritis. Takribani robo ya watu wanaopatwa na tatizo hili huwa hawana historia ya kuwa na ugonjwa wowote wa figo hapo kabla.
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kupata tatizo hili. Mambo hayo ni pamoja na: Matatizo katika mfumo wake wa damu, kuwahi kutumia vimiminika vilivyotengenezwa kwa kemikali za hydrocarbon, wenye historia ya saratani, maambukizi ya bakteria aina ya streptococcus, virusi, majipu au maambukizi katika moyo.
Mambo mengine ni yanayoweza kuongeza hatari ya kupatwa na tatizo hili ni pamoja na: Magonjwa ya mishipa ya damu kama vile vasculitis au polyarteritis, matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kutuliza maumivu za jamii kama vile aspirin, magonjwa ya mfumo wa kinga ya mwili , makovu katika chujio, au hali ya chujio kuwa na kuta nene kuliko kawaida na magonjwa yanayoathiri viungo mbalimbali vya mwili.
DALILI
Dalili kuu za chujio za figo kufa ni kuwa na damu katika mkojo (hali inayoufanya mkojo kuwa na rangi kama nyeusi, kutu au samawati; mkojo kuwa kama wenye povu jingi (kwa sababu ya kuwa na protini nyingi kuliko kawaida) na kuvimba uso, macho, miguu au tumbo hali inayojulikana kama edema.
Dalili nyingine ni pamoja na maumivu ya tumbo, kutapika damu, kuharisha au kupata choo kikubwa chenye kuchanganyika na damu, kupumua kwa shida, kukojoa kupita kiasi, homa. maumivu ya misuli na viungo, uchovu, maumivu ya mwili mzima pamoja na kukosa hamu ya kula na kutokwa na damu puani.
Baada ya muda, figo hushindwa kufanya kazi na mgonjwa huanza kuwa na dalili za mtu mwenye ugonjwa sugu wa figo. Kwa kawaida tatizo la uharibifu wa chujio za figo hutokea taratibu sana hali inayoweza kufanya ugunduzi wake kuchelewa pia. Wengi wa wagonjwa wenye tatizo hili hugunduliwa pale wanapokwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo mengine. Mara nyingi hali hii hujidhihirisha kwa kuwepo na hitilafu katika kipimo cha urinalysis.
Mambo makuu matatu yanaweza kuonesha kuwepo kwa uharibifu katika chujio za figo ni upungufu wa damu (anemia) na shinikizo la damu kuwa juu na ishara za kupungua kwa utendaji kazi wa figo.Vipimo vinavyoweza kufanywa hujumuisha vipimo vya mkojo, damu pamoja na picha kama vile Ultrasound, CT au SPECT/CT.
Vipimo vya mkojo kama vile urinalysis husaidia kuonesha:Utendaji kazi wa figo yaani Creatinine clearance pamoja na Urine creatinine, uchunguzi wa mkojo kwa kutumia hadubini, kuangalia kiasi cha protini katika mkojo na tindikali ya urea katika mkojo, chembe nyekundu za damu (RBC) katika mkojo na kiasi cha chumvi kwenye mkojo (yaani urine osmolality).
Ili kuthibitisha uwepo wa tatizo hili na aina yake, kipimo cha biopsy (renal biopsy) hutumika.Matibabu Matibabu ya kuharibika kwa chujio la figo hutegemea sana na kisababishi cha tatizo hili, aina yake pamoja na ukubwa wa tatizo lenyewe yaani wingi wa dalili pamoja na uzito wake.
Dalili ya muhimu sana kuithibiti ni ongezeko la shinikizo la damu ingawa kwa kawaida huwa ni ngumu sana kuthibiti shinikizo la damu kuwa katika kiwango cha kawaida. Mgonjwa anashauriwa pia kupunguza kiasi cha chumvi katika chakula chake na pia kiasi cha protini na maji anayokunywa ili kusaidia utendaji kazi wa figo.
Iwapo figo zitashindwa kufanya kazi kabisa, mgonjwa anaweza kuhitaji kufanyiwa dialysis au kupandikizwa figo mpya. Kudorora kwa chujio za figo kunaweza kusababisha kupungua kwa utendaji kazi wa figo au ugonjwa sugu wa figo kushindwa kufanya kazi, au kufa kabisa kwa figo zote (end-stage renal disease).
Uharibifu katika chujio za figo unaweza kusababisha mlingano usio sawa wa madini katika damu (electrolytes imbalance) kama vile ongezeko la madini ya potassium (hyperkalemia); maambukizi yanayojirudia katika njia ya mkojo, mrundikano wa maji mwilini hali inayoweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi au maji kujaa katika mapafu.
The post HATARI YA KUHARIBIKA KWA CHUJIO ZA FIGO (GLOMERULONEPHRITIS) appeared first on Global Publishers.
No comments: