HATIMA YA DHAMANA YA KESI INAYOWAKABILI MWENYEKITI WA CHADEMA PAMOJA NA MBUNGE WA TARIME BADO IKO CHINI YA MAHAKAMA YA RUFANI NCHINI

 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akitoka Mahakama leo Februari 18, 2019.

 Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii 

MAHAKAMA ya Rufani nchini inaendelea kushikilia hatima ya dhamana ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko baada ya jopo la Majaji watatu wa Mahakama hiyo kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) na kusema watatangaza siku ya kutolewa kwa uamuzi.

Jopo la Majaji likiongozwa na Mwenyekiti wao, Jaji Stella Mgasha, Mwanaisha Kwariko na Gerald Ndika, Leo Februari 18, 2019  wamesema uamuzi huo utatolewa baada ya kusikiliza hoja za upande wa mashitaka na upande wa utetezi zilizowasilishwa mahakamani hapo. Novemba 23, 2018 Jaji Wilbard Mashauri akiwa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, alifuta dhamana ya Mbowe na Matiko kutokana na kukiuka masharti ya dhamana.

Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko

Hata hivyo, washtakiwa hao walikata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi wa Kisutu kufuta dhamana yao ambapo rufani yao ilipangwa kwa Jaji Sam Rumanyika nae baada  kusikiliza mapingamizi ya pande zote iliamua kuanza usikilizaji wa rufaa hiyo.

Hata hivyo,  DPP alikata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama Kuu kukubaliwa kusikiliza rufaa hiyo. 

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, upande wa DPP, umewakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi na Paul Kadushi, huku upande wa wajibu rufani ukiongozwa na Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala, Jeriamiah Ntobesya na Rugemeleza Nshala.

Akiwasilisha hoja tatu za upande wa serikali,  wakili Nchimbi ameeleza katika hoja yao ya kwanza kuwa Jaji Sam Rumanyika, alipotoka kisheria kuhusu kukubali na kupanga usikilizwaji wa rufaa ya Mbowe na Matiko ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu kupinga dhamana yao.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Edward Lowassa akiwasili Mahakamani hapo kusikiliza kesi inayomkabili Mwenyekiti wake pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini.


Pia hoja nyingine ya pili ambayo Majaji walimtaka Nchimbi aiondoe ni kwamba Jaji Rumanyika alipendelea kwa kupotoka kisheria ambapo alilazimisha usikilizwaji wa Rufani wakati akijua kuna ukiukwaji wa kisheria.

Hata hivyo Jaji Mgasha alimuuliza Nchimbi kwa jinsi gani Jaji Rumanyika alipendelea na je kitu kisichozumgumzwa katika Mahakama Kuu, je Mahakama hiyo inaweza kuijibu...?

Kufuatia hayo,  Nchimbi aliiondoa hoja hiyo na kubakiwa na hoja mbili.

Katika hoja ya pili, Nchimbi alidai Mahakama Kuu haikuwapatia haki ya kutosha ya kusikilizwa na kwamba kunyimwa kwa haki hiyo ya kusikilizwa kunaonesha kuwa Jaji alipotoshwa kisheria kwa kuwanyima waomba rufaa haki ya kusikilizwa.

Ameendelea kudai kuwa siku ya kwanza kufika mahakamani waliwasilisha maombi ya kupatiwa muda wa kutosha wa kujiandaa ili kujitetea katika rufaa ya (Mbowe na Matiko) lakini hawakupatiwa muda wa kufanya hivyo kwani uamuzi ulisomwa saa 6 badala ya saa 8  hali iliyosababisha kushindwa kujiandaa kuwasilisha mapingamizi yao.


"Katika mchakato wa rufaa haki ya kusikilizwa ni muhimu na itaonekana mchakato wake utakapoonekana. Ni maoni yangu kuwa Jaji Rumanyika alikuwa na upendeleo na alijikuta anaangukia kwenye upotofu wa sheria wa kuendelea na rufaa hiyo,’’ alidai.

Aidha, ameiomba mahakama ione kwamba rufaa iliyopo Mahakama Kuu ina mapungufu na haipo sahihi kuwepo na kwamba inafaa kuondolewa ili warufani waweze kufuata utaratibu kwa mujibu wa sheria.

Katika hoja yake ya tatu, amedai Mahakama Kuu haikuzingatia haki ya kutosha ya kuwasikiliza.

Hata hivyo,  Jopo la Majaji walimuuliza ni sehemu gani inayoonyesha wamenyimwa haki ya kusikilizwa.

Wakili Nchimbi akadai, walinyimwa baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kusikiliza Rufaa ya Mbowe na Matiko.

Akijibu hoja Hizo,  wakili wa Utetezi Peter Kibatala ameiomba Mahakama hiyo itupilie mbali rufani hiyo kwa kuwa imeletwa bila sababu za msingi, kwani hata warufani wenyewe wamekiri katika hoja yao ya kwanza. 

Kwa upande waje,  Dk.Nshala amedai kuwa ni rai yao kwamba Warufani walipewa muda wa kutosha wa kusikilizwa na kwamba rufani iliyoletwa hapa imeletwa kwa nia mbaya na kuomba mahakama itupiliwe mbali.
Baada ya kutoa hoja hizo, Jaji Mgasha alisema mahakama imesikiliza hoja za pande zote mbili na itapanga tarehe kwa ajili ya kutolewa kwa uamuzi.

Mbali na Mbowe na Matiko, washitakiwa wengine katika kesi ya msingi ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.

No comments: