WATU SITA AKIWEMO MTOTO MCHANGA WAFA, SABA WAJERUHIWA KATIKA AJALI MSATA MKOANI PWANI

Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Watu sita akiwemo mtoto mchanga wa jinsia ya kike wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kijiji cha Msata, barabara kuu ya Segera/Chalinze mkoani Pwani. Akithibitisha, kamanda wa polisi mkoani Pwani Naibu Kamishna wa Polisi ACP Wankyo Nyigesa alisema kwamba ajali hiyo imetokea Novemba 5, 2018 majira ya saa moja usiku baada ya gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster ikitokea Mkata kwenda Mbezi -Dar es salaam kuligonga kwa nyuma lori namba KBV 746C/ZE2861 FAW iliyokuwa imeegeshwa barabarani kutokana na kuharibika. 
Amesema dereva wa Toyota coaster iliyosababisha ajali ambae hajafahamika jina lake alikimbia baada ya kutokea ajali. 
ACP Wankyo alieleza kuwa waliopoteza maisha ni wanaume watano wenye umri kati ya miaka 30-40 ambao majina yao bado kufahamika Alisema ,watu saba walipata majeraha kwenye maeneo mbalimbali ya mwili yao . 
"Waliopata majeraha ni pamoja na wanaume wanne na wanawake watatu ambao wote wamepelekwa zahanati ya jeshi Kihangaiko -RTS na kituo cha afya Lugoba kwa matibabu zaidi "alisema Wankyo, akiongesza kuwa  miili ya marehemu imehifadhiwa hospital ya wilaya ya Bagamoyo kwa uchunguzi wa daktari. 
 Alitaja chanzo cha ajali, ni uzembe wa dereva wa gari namba T. 124 DHW aina ya Toyota coaster kujaribu kulipita bila tahadhari gari jingine lililokuwa limeegeshwa baada ya kuharibika na wanaendelea kumsaka. 
Kamanda huyo alitoa rai kwa madereva kutii sheria za usalama barabarani na kuacha tabia za kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi ili kuepukana na ajali zembe. Wankyo aliwapa salamu madereva hao, kuwa hawatakuwa na muhali nao kwani watakamatwa na kuwachukulia hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine. 
Kwa upande wao mashuhuda wa ajali hiyo akiwemo mwenyekiti wa kitongoji cha Pugini, kijiji cha Msata Siasa James alisema hii ni ajali mbaya ambayo haijawahi kutokea eneo hilo. 
 "Tulisikia mshindo, na kuona tukimbilie eneo la tukio ndipo tulipokuta gari ya abiria imelivaa lori kwa nyuma na kisha kukatika upande wa kondakta "alieleza. 
 Nae Stephen Hinjo alieleza kwamba, gari ya abiria walikutana nayo ambapo ilipita hata dakika mbili hazijapita walisikia kishindo na kutahamaki waliona limekwenda kujikita nyuma ya lori lililokuwa limepaki pembeni mwa barabara. 
 "Kufika eneo la tukio tulikuta abiria upande wa kondakta umebanwa huku vichwa viwili vikiwa vinaning'inia chini, wengine wamekatika mikono na shingo, ni ajali haijawahi tokea, "kikubwa tulichokifanya ni kuopoa miili na polisi walifika eneo la tukio "alifafanua Hinjo.
Kamanda wa polisi mkoani Pwani Naibu Kamishna wa Polisi ACP Wankyo Nyigesa na wasaidizi wake wakiwa eneo la ajali
Kamanda wa polisi mkoani Pwani Naibu Kamishna wa Polisi ACP Wankyo Nyigesa na wasaidizi wake wakiwa eneo la ajali

No comments: