Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la kitaifa la ustawi wa Jamii ,katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi.
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano hilo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa kongamano la kitaifa la ustawi wa Jamii.
Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO) ,Zena Mabeyo akizungumza wakati wa kongamano hilo.
Baadhi ya Washiriki katika kongamano hilo.
Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, Ummy Mwalimu ,akiteta jambo na Kamishna wa Ustawi wa Jamii nchini Dkt Naftali Ng’ondi wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, Ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Kongamano hilo lililofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi .
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii ,Kanda ya Kaskazini ,Moshi
Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto, Ummy Mwalimu amesema kukamilika kwa mchakato wa sheria ya kusimamia kada ya maafisa ustawi wa jamii nchini itasaidai kurudisha hadhi na heshima kwa kada hiyo likiwemo suala la maadili pamoja na utendaji kazi.
Waziri Mwalimu amesema kukosekana kwa sheria hiyo kumepelekea baadhi ya maafisa ustawi wa jamii kukosa uadilifu ikiwemo kujihusisha katika vitendo vya rushwa pamoja na kushindwa kutoa haki kwa usawa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kungamano la Kitaifa la ustawi wa jamii, lililofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hospitali ya rufaa ya KCMC Mjini Moshi, amesema kupatikana kwa sheria hiyo pia kutawezesha ufutaji wa leseni kwa wale watakaoenda kinyume na sheria..
Katika Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu ya mchango wa taaluma ya ustawi wa jamii katika kuelekea uchumi wa viwanda na maendleo endelevu,Waziri Mwalimu alisema sheria hiyo itajumuisha suala la usajili wa kwa maafisa ustawi wa jamii ili kusimamia maadili na weledi katika kazi zao .
Alisema kuwa wapo baadhi ya wananchi wenye kipato cha chini wameshindwa kufika katika ofisi za ustawi ngazi za Halmashauri kwa sababu imeshajengeka dhana kuwa mwenye fedha ndiye anaesikilizwa na kupewa haki.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wataalamu wa ustawi wa jamii Tanzania (TASWO) ,Zena Mabeyo amesema kuwa kuwepo kwa chombo maalumu kwa ajili ya kada hiyo kitakuwa na nafasi kubwa katika kusimamia masuala mazima ya maadili na kuchukua hatua kwa wasiofuata sheria.
Naye Kamishna wa ustawi wa jamii nchini Dkt Naftali Ng’ondi amesema ni muhimu uwepo wa sheria mahsusi itasaidia kuchukua hatua kwa baadhi ya watendaji wanaofanya kazi za ustawi wa jamii huku wakiwa hawajasomea taaluma hiyo.
No comments: