TRAMEPRO YATOA RAMBIRAMBI KWA WAATHIRIKA WA AJALI ZA BARABARANI MOROGORO
Dar es Salaam, Oktoba 10, 2026
Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kufuatia ajali za barabarani zilizoripotiwa kutokea mkoani Morogoro.Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo, imeeleza kuwa shirika hilo limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo na majeruhi kutokana na ajali hizo, huku likitoa pole kwa familia zilizofikwa na msiba huo.
TRAMEPRO pia imewaombea majeruhi kupata matibabu yanayostahili na kupona haraka, huku ikiomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi na kuwapa wafiwa nguvu na faraja katika kipindi hiki kigumu.
Katika taarifa hiyo, TRAMEPRO imeungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa pole kwa familia zilizofiwa na kuhimiza wananchi kuzingatia sheria na tahadhari za usalama barabarani.
Aidha, shirika hilo limetoa wito kwa Serikali kuendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia ajali, kuboresha usalama wa miundombinu na kuhakikisha huduma za dharura zinawafikia waathirika kwa wakati.
TRAMEPRO pia imezitaka mamlaka za usalama barabarani kuongeza elimu kwa umma, kudhibiti mwendo kasi na uendeshaji hatarishi, pamoja na kufanya uchunguzi wa kitaalamu wa ajali ili kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wa madereva na watumiaji wengine wa barabara, shirika hilo limesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, kukagua hali ya magari na kuepuka vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha.
TRAMEPRO imesisitiza kuwa usalama barabarani ni wajibu wa kila mmoja na kwamba ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya usalama, sekta ya afya, vyombo vya habari, wadau wa usafirishaji na wananchi ni muhimu katika kupunguza ajali, vifo na majeruhi nchini.
“Kulinda maisha ni wajibu wetu sote. Tuheshimu sheria, tuwe waangalifu, tulinde maisha,” imeeleza taarifa hiyo.
Imetolewa na:Boniventura Mwalongo Katibu Mkuu, TRAMEPRO
No comments: