SPIKA WA UINGEREZA AMPENDEKEZA ZUNGU KUWA RAIS WA MKUTANO WA 153 WA IPU
Na Mwandishi wetu
Katika hali inayoonesha kuwa mataifa makubwa duniani yameendelea kuonesha imani kubwa kwa Tanzania, Spika wa Bunge la Wawakilishi la Uingereza (House of Commons) Mhe. Sir Lindsay Hoyle, amempendekeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa Umoja Mabunge Duniani (IPU).Sir Lindsay amempendekeza Spika Zungu leo Oktoba 6, 2026 asubuhi wakati wa kikao ambapo awali, Rais wa IPU Mhe. Dkt. Tulia Ackson aliwaeleza wajumbe kuwa wanapaswa kumchagua Rais wa Mkutano huo wa 153 unaoendelea jijini Arusha.
Baada ya maelezo ya Dkt. Tulia kuhusu kumchagua Rais wa mkutano huo, Spika wa Bunge Bunge la Wawakilishi la Uingereza Mhe. Sir Lindsay Hoyle alitoa hoja na kumpendekeza Spika Zungu.
“Ninayo furaha na heshima kubwa ninampendekeza Spika wa Tanzania achaguliwe kuwa Rais wa Mkutano wa 153. Ninapenda kusema kuwa urafiki huenda mbali, urafiki ni wa ndani na ndio maana ni heshima kubwa kuwa naweza kumpendekeza Spika kutoka Tanzania”, alieleza Spika Lindsay na kutoa hoja.
Pendekezo hilo liliungwa mkono na mjumbe kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na mjumbe kutoka Uganda na hatimaye kuunwa mkono na wajumbe wote wa kikao hicho.
Akiongea baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano wa 153 wa IPU, Mheshimiwa Zungu aliwashukuru wajumbe kwa kumchagua na kueleza kwamba amekubali kushika nafasi hiyo kwa moyo mmoja.
“Mheshimiwa Rais wa IPU na wajumbe wote wa Mkutano huu, kwa moyo wa dhati, nawashukuru wajumbe wote, Tanzania inajivunia kuwakaribisha jijini Arusha na tutaendelea kuwa pamoja katika mkutano huu wa 153 wa IPU” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa IPU na Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania alimpongeza Mhe. Zungu kuwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Mkutano huo wa 153 wa IPU.

No comments: