MZOZO MASHARIKI YA KATI WAPAISHA BEI YA MAFUTA BAADA YA KUSHUKA MIEZI MITATU



Na Mwandishi Wetu

BAADA ya bei za mafuta kushuka kwa miezi mitatu mfululizo, bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini imeongezeka kuanzia leo, Jumatano, Oktoba 7, 2026, kutokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizo katika soko la dunia.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli zitakazotumika nchini kuanzia saa 6:01 usiku wa leo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ongezeko hilo limetokana na mabadiliko ya bei katika soko la dunia, ikiwamo kuibuka upya kwa mgogoro wa kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati, ambako Tanzania hununua sehemu kubwa ya bidhaa zake za mafuta.

Mzozo huo umeathiri uzalishaji, upatikanaji na usafirishaji wa mafuta duniani, hali iliyosababisha kupanda kwa bei ya bidhaa za mafuta yaliyosafishwa katika soko la kimataifa.

Kutokana na mwenendo huo, bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini kwa mwezi Oktoba 2026 zimeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita.

Serikali imesema inaendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha bidhaa za mafuta zinaendelea kupatikana nchini kwa uhakika, licha ya mabadiliko ya bei katika soko la dunia.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa soko la mafuta duniani na kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji endelevu wa bidhaa hizo pamoja na bei himilivu kwa wananchi.

Kwa mujibu wa bei mpya za EWURA, jijini Dar es Salaam, bei kikomo ya rejareja kwa lita moja ya petroli ni Sh4,057, dizeli Sh4,086 na mafuta ya taa Sh4,067.

Mkoani Tanga, bei kikomo ya rejareja kwa lita moja ya petroli ni Sh4,123, dizeli Sh4,152 na mafuta ya taa Sh4,133.

Mtwara, bei kikomo ya rejareja kwa lita moja ya petroli ni Sh4,170, dizeli Sh4,199 na mafuta ya taa Sh4,180.

EWURA imewakumbusha wananchi kuhakikisha wanachukua risiti kila wanaponunua mafuta ili kuwa na uthibitisho wa manunuzi yao.

No comments: