MKUYU AFRICA YAWATAKA MADALALI KUJITAMBUA, KUEPUKA KUCHUKULIWA KAMA ‘VISHOKA’
DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Mkuyu Africa imewataka madalali wa nyumba na ardhi nchini kuzingatia maadili ya kazi, kujiendeleza kitaaluma na kujiunga na mifumo rasmi ya usajili ili kujenga uaminifu kwa wateja na kurejesha heshima ya taaluma hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mkuyu Africa, Juneid Othman, wakati wa mkutano uliowakutanisha madalali na wadau wa sekta hiyo kujadili changamoto zinazowakabili pamoja na umuhimu wa kuanzisha mfumo rasmi wa kuwatambua na kuwasimamia.
Juneid alisema sekta ya nyumba, ardhi na ujenzi ina mchango mkubwa katika maisha ya wananchi, hivyo inahitaji watu wenye uaminifu, weledi na uwajibikaji ili kulinda maslahi ya wateja na kuimarisha imani ya umma.
Alisema licha ya kuwepo kwa madalali wengi wanaofanya kazi kwa uaminifu, baadhi ya watu wamekuwa wakijihusisha na shughuli za udalali bila utambulisho rasmi wala mfumo wa kuwawajibisha wanapokiuka maadili, hali inayochangia malalamiko na kuharibu taswira ya taaluma hiyo.
“Tatizo linapotokea kwa mtu mmoja, wakati mwingine jamii inawaona madalali wote kama vishoka. Hali hii inawanyima heshima wale wanaofanya kazi kwa uaminifu na weledi,” alisema Juneid.
Alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Bodi ya Madalali itakayoweka viwango vya kitaaluma, kusimamia maadili na kusaidia kutambua madalali wanaofanya kazi kihalali ndani na nje ya nchi.
Alisema mfumo huo utasaidia pia kuwalinda wateja dhidi ya utapeli na migogoro inayoweza kujitokeza wakati wa kununua, kuuza au kupanga nyumba na ardhi.
“Tunapokwenda kwa daktari, wakili au mkandarasi, kuna mifumo inayotuwezesha kutambua na kufuatilia wataalamu hao. Madalali nao wanahitaji mfumo utakaowatambua na kuwaweka katika viwango vinavyokubalika,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama cha madalali nchini, Emmanuel Machibya, alisema kuanzishwa kwa bodi hiyo kutasaidia kuwaunganisha madalali na kuweka msingi wa kutambuliwa kisheria.
Alisema wazo la kuanzisha bodi hiyo limepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi na wadau mbalimbali baada ya Mkuyu Africa, kupitia jukwaa la Miliki Mali, kuibua umuhimu wa kuwa na chombo kitakachosimamia taaluma hiyo.
Machibya alisema bodi hiyo inatarajiwa kusaidia kulinda haki na maslahi ya wateja pamoja na wanunuzi, huku ikiwapa madalali mfumo wa kufanya kazi kwa uwazi na uwajibikaji.
Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Leonida Sudi Ibrahim, aliiomba Serikali kuweka utaratibu wa kuwatambua na kuwarasimisha madalali ili waweze kufanya kazi katika mfumo unaotambulika kisheria.
Alisema chama hicho kimejipanga kutoa elimu na mafunzo kwa madalali katika maeneo mbalimbali nchini, kwa msisitizo maalumu kwa wanawake, ili kuwajengea uwezo, kujiamini na kuzingatia misingi ya taaluma.
Ibrahim alisema kupitia mwamvuli wa TBAB, wanatarajia kuanzisha mfumo maalumu wa utambulisho wa madalali na kuendesha mafunzo yatakayowasaidia kuboresha utendaji wao na kuelewa wajibu wao kwa wateja.
Aliwataka madalali wanawake kutokata tamaa kutokana na changamoto wanazokutana nazo, akisema wana uwezo wa kushindana katika sekta hiyo iwapo watajiamini, kujitambua na kutumia fursa zilizopo.
Aliongeza kuwa umoja na urasimishaji wa shughuli zao unaweza kuwasaidia madalali kupata fursa za huduma za kifedha na mikopo kutoka taasisi husika, hatua itakayochangia kuimarisha biashara zao na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa chama Cha Madalali ,Emmanuel Machibya akizungumza wakati wa mkutano wa chama hicho jijini Dar es salam
.jpeg)

No comments: