TAPSEA YAPATA UONGOZI MPYA, LEAH MWAMBA AOMBA WANACHAMA USHIRIKIANO

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Viongozi wapya wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA) wameapishwa rasmi jijini Dar es Salaam, huku wakitakiwa kusimamia Katiba ya chama na kulinda maslahi ya wanachama katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza wakati wa kuwaapisha viongozi hao, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga, aliwataka kuzingatia Katiba ya TAPSEA na kuitumia kama mwongozo katika uongozi wao ili kuhakikisha wanachama wanaongozwa kwa haki na ufanisi.

Kiswaga amesema TAPSEA ni chama kikubwa chenye wajibu wa kuwatumikia wanachama wake, hivyo viongozi wanapaswa kuwa imara katika kusimamia maslahi yao na kuhakikisha chama kinaendelea kusonga mbele.

“Niwaombe viongozi mnapotoka hapa mkasimamie vyema Katiba yenu ili kuweza kuondoa migogoro itakayojitokeza,” alisema Kiswaga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa TAPSEA, Leah Mwamba, aliwashukuru wanachama kwa kumpa dhamana ya kuwaongoza na kuahidi kushirikiana nao katika kuhakikisha chama kinafikia malengo yake. Amesema tukio la uapisho ni hatua muhimu katika safari ya uongozi na kuomba wanachama waendelee kuwaunga mkono.

“Ninatoa shukrani zangu za pekee kwa wote walioungana nasi katika historia hii. Jambo hili la uapisho ni kubwa sana, hivyo tunaomba mzidi kutuombea tufanye vyema katika uongozi,” alisema Mwamba.

Naye Katibu Mkuu wa TAPSEA, Hellen Magati, aliwashukuru wageni na wadau waliohudhuria hafla hiyo, akiahidi kuwa uongozi mpya utashirikiana na wanachama na wadau mbalimbali katika kutekeleza majukumu yake na kuimarisha chama.

Viongozi wengine walioapishwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Zainab Ibrahim Ally, Naibu Katibu Mkuu, Halima Twaha Mgulo, Mweka Hazina, Nyanza Msongela, pamoja na wajumbe wengine waliochaguliwa katika uongozi huo.












No comments: