TANZANIA NA MAREKANI ZAAZIMIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI

 



WAZIRI  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo wamefanya mazungumzo na ujumbe maalum wa Wajumbe 11 wa Baraza la Wawakilishi la Marekani (Congress) kutoka Vyama vyote viwili Vikuu nchini Marekani, ulioongozwa na Mhe. Ronny Jackson, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya ya Huduma za Kijeshi, Ulinzi na Usalama ya Baraza la Wawakilishi la Marekani (House Armed Services Subcommittee).

Mazungumzo hayo yaliyofanyika tarehe 27 Julai 2026 katika Ofisi za Makao Mkuu ya zamani ya Jeshi la Wananchi la Tanzania, Ngome Upanga, Dar es Salaam, yalilenga kujadili maeneo ya kipaumbele katika uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, hususan ushirikiano wa biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama pamoja na hali ya amani na usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakati wa mazungumzo hayo, ilionyesha dhamira ya kupanua ushirikiano katika biashara na uwekezaji, hususan katika sekta za kimkakati zikiwemo gesi asilia (LNG), Madini muhimu, usafiri wa anga, ulinzi na usalama.

Aidha, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano baina ya wananchi wa nchi hizo mbili kwa kuondoa vikwazo vya visa kwa Watanzania wanaosafiri kwenda Marekani pamoja na Vikwazo vyengine ambavyo Marekani iliiwekea Tanzania.

Ujumbe wa Marekani uliipongeza sana Tanzania kwa mchango wake katika kudumisha amani na usalama wa kikanda, ikiwemo juhudi za kupambana na ugaidi na ushiriki katika operesheni za kulinda amani barani Afrika.

Pande hizo mbili zilikubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika maeneo yenye maslahi ya pamoja na pia kukubali kupitia tena maombi yote ya Vikwazo hivyo yaliyowasilishwa Rasmi na Tanzania na kukubaliana kukutana tena katika Vikao Vijavyo vitakavyofuata kwa lengo la ufuatiliaji kati ya Nchi mbili.

Kikao hicho kilikuwa na mafanikio makubwa kwa hatua hiyo ya awali.



No comments: