PROFESA PALLANGYO :TIA INAWAJENGA VIJANA KWA AJIRA ZA KIDIJITALI
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA) imesema kuwa katika karne ya sasa teknolojia ni nyenzo muhimu ya maendeleo, hivyo imejikita katika kuwawezesha vijana kutumia maarifa na ubunifu wa kidijitali kutengeneza suluhisho za changamoto zinazowakabili wananchi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, alisema hayo alipotembelea banda la Taasisi hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Profesa Pallangyo amesema maonesho hayo ni fursa kwa wananchi kujifunza kuhusu elimu, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia katika kilimo, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.
Alisema TIA imeshiriki maonesho hayo kwa kuwaleta wataalamu na wanafunzi wake kwa lengo la kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara kuhusu uhasibu, utunzaji wa fedha na kumbukumbu, masoko, ugavi pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji na biashara.
Kwa mujibu wa Profesa Pallangyo, moja ya vivutio katika banda la TIA ni ubunifu wa wanafunzi kutoka Kampasi za Mwanza na Kigoma, ambao wamebuni mifumo ya kidijitali inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na wafanyabiashara.
“Lengo letu si kuwafundisha wanafunzi wapate ajira pekee, bali kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia ubunifu. Ndiyo maana tumeanzisha kitengo maalumu kinachowasaidia kubuni teknolojia na biashara zinazotatua changamoto za jamii,” amesema.
Aliongeza kuwa TIA imejumuisha matumizi ya teknolojia na Akili Bandia (Artificial Intelligence) katika mitaala yake ili kuwawezesha wanafunzi kubuni suluhisho zinazokidhi mahitaji ya soko na kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.
MIZANI YA KIDIJITALI KUMKOMBOA MKULIMA
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa TIA Kampasi ya Mwanza, Paschal Sabuni Shija, alisema amebuni mfumo wa mizani ya kidijitali unaotumia nishati ya jua na kuunganishwa na stakabadhi za EFD pamoja na teknolojia ya Akili Bandia kwa ajili ya kuboresha ununuzi wa pamba na mazao mengine.
Amesema mfumo huo unamwezesha mkulima kupata uzito sahihi wa mazao yake, kupokea risiti na ujumbe mfupi wa simu mara baada ya mauzo, huku ukitoa taarifa za bei ya soko kwa wakati halisi.
Shija alisema ubunifu huo pia unalenga kupunguza udanganyifu unaoweza kujitokeza katika matumizi ya mizani ya kawaida.
“Kwa kupitia mfumo huu, mkulima anapata haki yake kwa sababu mizani haiwezi kuchezewa. Serikali pia inapata taarifa sahihi kwa wakati na wafanyabiashara wanafanya kazi kwa uwazi zaidi,” alisema.
BIZPOWER KUSAIDIA USIMAMIZI WA BIASHARA
Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa TIA Kampasi ya Kigoma, Daud Temaunji, alisema amebuni mfumo wa BizPower unaowawezesha wafanyabiashara, wakulima na wajasiriamali kusimamia shughuli zao za biashara kwa njia ya kidijitali wakiwa mahali popote.
Amesema mfumo huo unamwezesha mtumiaji kupata taarifa za mauzo, manunuzi, bidhaa zilizopo stoo na taarifa nyingine muhimu kupitia simu au kompyuta.
Daud alisema mfumo huo una uwezo wa kufanya kazi hata bila huduma ya intaneti, jambo linalowawezesha watumiaji kuendelea kusimamia biashara zao katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa mtandao.
Hata hivyo amseema ubunifu huo unalenga kuwasaidia wafanyabiashara kufanya maamuzi kwa haraka, kuboresha usimamizi wa biashara na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku.


.jpeg)
.jpeg)
No comments: