PPAA YAHIMIZA WAZABUNI KUTUMIA MODULI YA MALALAMIKO NA RUFAA KATIKA MFUMO WA NeST
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imewahimiza wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma kutumia Moduli ya Kupokea na Kushughulikia Malalamiko na Rufaa katika mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) kuwasilisha malalamiko na rufaa zao PPAA pindi wanapoona hawakutendewa haki katika michakato ya ununuzi wa umma.
Akizungumza na waandishi wa Habari pembezoni mwa Kongamano la kumi la ununuzi wa Umma la mwaka 2026 linaloendelea Jijini Arusha kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma PPAA, Bw. Nelson Kessy amesema kuanza kwa matumizi ya Moduli hiyo kuna faida nyingi kama vile kuokoa muda na gharama.
“Faida nyingine za wazabuni na taasisi nunuzi kutumia moduli ni pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu sahihi za malalamiko na rufaa zinazowasilishwa na wazabuni, na kuongeza ufanisi katika utoaji wa uamuzi,” amesema Bw. Kessy
Bw. Kessy ameongeza kuwa Mamlaka ya Rufani inawaelekeza wazabuni wote wa ndani na nje ya nchi kutumia Moduli ya kuwasilisha Malalamiko na Rufaa kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na kanuni zake pindi wanapoona hawakutendewa haki katika zabuni walizoomba.Katika hatua nyingine, Bw. Kessy amesema kuwa PPAA inatoa huduma ya Mkutano kwa njia ya Mtandao “Video Conference” ambapo hutumika kusikiliza mashauri ya wazabuni walioshindwa kufika moja kwa moja katika Ofisi za PPAA kwa ajili ya kusikiliza mashauri yalilowasilishwa mbele yake.
Huduma ya Mkutano kwa njia ya Mtandao imetoa fursa ya kuwasikiliza wazabuni walioshindwa kufika PPAA kutokana na sababu mbalimbali na kuiwezesha Mamlaka ya Rufani kutekeleza jukumu lake la msingi la utatuzi wa migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa Umma.
“Tangu kuanza kwa matumizi ya ‘video conference’ tayari PPAA imewasikiliza wazabuni mbalimbali kutoka katika mataifa ya Afrika Kusini, Nigeria, Poland, India na China,” amesema Bw. Kessy.
Kadhalika, Mamlaka ya Rufani inatarajia kuunganisha Moduli ya Malalamiko na Rufaa na mfumo wa Mahakama ya Tanzania ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma ikiwa ni njia mojawapo ya kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya ununuzi wa umma.
Naye mzabuni Peter Sarungi kutoka makundi maalum alisisitiza sekta ya makundi maalum ipewe kipaumbele zaidi katika uombaji wa zabuni na kufuatilia taasisi zilizotangaza zabuni ili wapewe taarifa kama wamepata zabuni au la ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi ikiwemo kutumia Moduli ya PPAA.
Matumizi rasmi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST yalianza mwezi Februari, 2025.



No comments: