Miaka 37 ya MSI Tanzania yatajwa kuchangia kupunguza vifo vya uzazi kwa asilimia 40
Na Karama Kenyunko
UTOAJI wa elimu ya afya ya uzazi, huduma za uzazi wa mpango na mafunzo kwa watoa huduma za afya wa serikali katika vituo vya afya umeelezwa kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga, mimba zisizotarajiwa na kuwasaidia wasichana na vijana kufikia ndoto zao katika kipindi cha miaka 37 ya shughuli za MSI Tanzania nchini.
Akizungumza Ijumaa wiki iliyopita katika maadhimisho ya miaka 37 ya MSI Tanzania tangu ilipoanza kutoa huduma nchini mwaka 1989, Mratibu Msaidizi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, Agnes Mgaya, alisema miaka hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kupitia ushirikiano kati ya MSI Tanzania na Serikali.
"Miaka 37 siyo mchezo, kuna mabonde na milima. Kuna watu wengi wamejifunza kutoka MSI Tanzania. Nawapongeza watumishi wa MSI Tanzania hasa katika eneo la outreach programme (huduma ya M-koba), mmewezesha watu kupata huduma ya uzazi wa mpango, na pia mmeweza kufanya kazi na watoa huduma wa afya serikalini. Manesi shikizi (Embedded Nurses) wameweza kutoa mafunzo na watumishi hawa wamejifunza kutoka kwa manesi hawa wakiwa kazini na sasa wana uwezo wa kutoa huduma muda wowote kwa mteja katika vituo vyao vya afya," alisema.
Alisema afua zinazotekelezwa na MSI Tanzania kwa kushirikiana na Serikali zimechangia kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 40.
Mgaya alisema mbali na kutoa huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango, MSI Tanzania imekuwa ikitoa mafunzo kwa watoa huduma wa afya kuhusu namna ya kupanga mipango ya vituo vya afya, hatua ambayo itasaidia kuandaa na kutekeleza mipango inayochangia kuboresha afya ya watu binafsi na jamii, kuweka vipaumbele na kutumia rasilimali zilizopo kwa ufanisi.
---
Kwa upande wake, Mratibu wa Mkoa wa Afya ya Mama na Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam, Rehema Panga, aliipongeza MSI Tanzania kwa mchango wake katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto pamoja na mimba zisizotarajiwa.
"Pia tunatambua mchango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) na United Kingdom's Foreign, Commonwealth and Development Office (FCDO). Mchango wenu ni mkubwa sana. Kama Serikali tunawapongeza sana kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa akina mama na mtoto," alisema.
Alisema kwa mujibu wa tafiti, utoaji wa huduma za uzazi wa mpango unapunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 40.
Panga pia aliishukuru MSI Tanzania kwa kufika maeneo yasiyofikika kupitia huduma za M-koba, ambapo imeweza kuwafikia vijana kwa elimu pamoja na kuwapa elimu watu wenye ulemavu.
Naye Mkurugenzi wa MSI Tanzania, Patrick Kinemo, alisema shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali, washirika wa maendeleo na wadau wengine kuhakikisha wanawake na familia wanaendelea kupata huduma bora za afya ya uzazi na afya ya ngono licha ya changamoto za kifedha.
"Leo tunaadhimisha miaka 37 ya uwepo wa MSI nchini Tanzania na mchango wetu katika sekta ya afya, hususan afya ya uzazi na uzazi wa mpango," alisema.
Kinemo alisema kupungua kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili kumesababisha changamoto kwa programu za afya, lakini MSI imepanua vyanzo vya ufadhili na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati ili kuhakikisha huduma muhimu zinaendelea kutolewa bila kukatizwa.
Alieleza kuwa shirika hilo limeanzisha mfumo endelevu wa ufadhili unaochanganya misaada ya wafadhili na mapato yanayotokana na masoko ya kijamii pamoja na vituo vya afya, ambapo mapato kutoka hospitali na kliniki zinazohudumia wateja wanaolipia huduma pamoja na wenye bima ya afya hutumika kugharamia huduma za bure za afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa jamii zilizo katika mazingira magumu.
Aliongeza kuwa MSI Tanzania pia huuza bidhaa za afya ya uzazi kama kondomu, njia za uzazi wa mpango na vidonge vya dharura vya uzazi wa mpango, huku mapato hayo yakisaidia programu za huduma za M-koba katika maeneo ya vijijini na maeneo magumu kufikika.

Mwenyekiti wa Bodi ya MSI Tanzania, Magreth Ngasani, alisema ushirikiano wa shirika hilo na Serikali umechangia kuboresha afya ya mama na mtoto kwa kuunga mkono juhudi za kitaifa za kupunguza vifo vya akina mama vinavyoweza kuzuilika.
Alisema uzazi wa mpango unabaki kuwa moja ya hatua muhimu zaidi katika kupunguza vifo vya akina mama kwa kuwa unawawezesha wanawake kupanga na kutenganisha mimba kwa usalama huku ukipunguza hatari za kiafya.
Ngasani alisema mbali na utoaji wa huduma, MSI imekuwa ikiunga mkono programu za Serikali za huduma za M-koba kwa kutoa usafiri, rasilimali za kifedha na msaada wa vifaa unaowawezesha wahudumu wa afya kuwafikia wananchi katika maeneo yasiyofikiwa kwa urahisi.
Aliongeza kuwa shirika hilo pia limewekeza katika kuimarisha mifumo ya afya kwa kuwajengea uwezo wahudumu wa afya katika mipango na usimamizi pamoja na kusaidia vituo vya afya kuandaa mipango bora ya uendeshaji ya kila mwaka na kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Ofisi ya Uingereza ya Masuala ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO), Getrude Mapunda, aliipongeza MSI Tanzania kwa kubadili maisha ya wanawake, wasichana na jamii kupitia utoaji wa huduma za afya ya uzazi, hususan katika maeneo magumu kufikika nchini.
Alisema mafanikio yaliyopatikana katika kuendeleza haki za wanawake na huduma za afya ya uzazi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita yanakabiliwa na shinikizo kutokana na mabadiliko ya mazingira ya kisiasa na kijamii, hivyo kuendelea kuwekeza na kuimarisha ushirikiano ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Akikumbuka ziara zake katika jamii za mbali akiwa na timu za huduma za M-koba za MSI, Mapunda aliwapongeza wahudumu wa afya kwa kujitolea kwao licha ya mazingira magumu ili kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma zinazookoa maisha.
Alithibitisha tena dhamira ya Serikali ya Uingereza ya kuendelea kuunga mkono uwekezaji kwa vijana na kusisitiza kuwa uongozi imara wa Serikali, ushirikiano endelevu na kuendelea kuunga mkono huduma za afya ya uzazi ni mambo muhimu katika kuboresha matokeo ya afya na kuhakikisha jamii zinakuwa na mustakabali wenye afya bora.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
No comments: