Dkt. Nchimbi: Uchumi wa Viwanda ni Nguzo ya Tanzania Kufikia Hadhi ya Uchumi wa Juu wa Kati

 

Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Tanzania, Dkt.Emmanuel Nchimbi, amesema safari ya Tanzania kuelekea kuwa nchi yenye uchumi wa juu wa kati itategemea kwa kiwango kikubwa ujenzi wa uchumi wa viwanda wenye ushindani, huku akihimiza kuongezwa kwa uwekezaji katika ubunifu, teknolojia na uzalishaji wa bidhaa zenye thamani zaidi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya Tuzo za Jubilei ya kuadhimisha miaka 50 ya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Dkt. Nchimbi alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka ajenda ya maendeleo ya viwanda kuwa msingi wa mageuzi ya uchumi wa taifa kwa muda mrefu.

Alisema serikali imeendelea kutekeleza maboresho mbalimbali ya sera, kuimarisha miundombinu ya kimkakati, kufanya mageuzi ya taasisi na kuweka mazingira rafiki zaidi kwa biashara na uwekezaji ili kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi.

"Dhamira ya serikali ni kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani utakaoiwezesha Tanzania kufikia hadhi ya uchumi wa juu wa kati na kuongeza uwezo wa nchi kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa," alisema.

Dk. Nchimbi alisema maonesho ya Sabasaba yamekua kutoka kuwa tukio la kila mwaka la biashara na kuwa jukwaa muhimu linaloongeza ushindani wa biashara, kupanua masoko ya wazalishaji na kuimarisha uhusiano kati ya wazalishaji, wafanyabiashara na watumiaji.

Alisema ifikapo mwaka 2050, maonesho hayo yanapaswa kuwa miongoni mwa maonesho makubwa zaidi ya biashara duniani, yakiiweka Tanzania kuwa kitovu cha biashara, uwekezaji, ubunifu na maendeleo ya viwanda barani Afrika.

Aidha, aliwataka wazalishaji wa ndani kutumia kikamilifu nembo mpya ya Made in Tanzania, akisema itasaidia kuongeza utambulisho na ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya Afrika na dunia.

Makamu wa Rais alisisitiza kuwa ili kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, viwanda vinapaswa kuelekeza nguvu katika uzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa kwa kutumia teknolojia za kisasa zinazoongeza tija na ufanisi.

Pia alihimiza uwekezaji zaidi katika tafiti, ubunifu, akili bandia (AI), biashara za kidijitali na mifumo ya kisasa ya uzalishaji ili viwanda vya Tanzania viweze kushindana katika uchumi wa dunia unaoendeshwa na teknolojia.

Vilevile, Dkt.Nchimbi alizitaka taasisi za kifedha kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wazalishaji, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati (SMEs), akibainisha kuwa ukosefu wa mitaji ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha ukuaji wa sekta ya viwanda.

Nae Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga alisema mafanikio ya Maonesho ya Sabasaba yanaonyesha imani kubwa ya wawekezaji, wazalishaji na wafanyabiashara ambao wameendelea kuboresha ubora wa bidhaa na kutafuta masoko mapya ya nje.

Alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano imara kati ya serikali na sekta binafsi, huku wakulima, wazalishaji, wafanyabiashara, wabunifu na washirika wa maendeleo wakitoa mchango mkubwa katika kuifanya Sabasaba kuwa jukwaa la biashara la kitaifa na kimataifa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Tanzania Dkt.Latifa Khamis, alisema katika kipindi cha miaka 50, Maonesho ya Sabasaba yamewezesha fursa za biashara zenye thamani ya shilingi trilioni 129.2.

Alisema maonesho hayo yameendelea kuwa moja ya majukwaa makubwa ya kukuza biashara nchini kwa kuwaunganisha wafanyabiashara wa ndani na wawekezaji wa kimataifa, hivyo kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kimataifa.

Katika hafla hiyo ya miaka 50 ya kuanzishwa TanTrade , taasisi, kampuni na watu binafsi waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka 50 walitunukiwa tuzo maalumu kwa mchango wao katika kuendeleza viwanda, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa Tanzania

No comments: