‘’MPANGO WA SINZA SI WA KUWAONDOA WANANCHI’’-DKT AKWILAPO

Na Munir Shemweta, WANMM

Serikali imewahakikishia wakazi wa Sinza kuwa Mpango wa Uendelezaji Upya wa Eneo la Sinza wa mwaka 2026–2046 haulengi kuwaondoa wananchi katika maeneo yao, bali kuboresha matumizi ya ardhi, kuongeza thamani ya mali zao na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.

Akifungua Mkutano wa wadau kukusanya maoni kuhusu Rasimu ya Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Sinza jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amesema, mpango huo unalenga kuongeza thamani ya ardhi, kuboresha mazingira ya makazi, kuimarisha miundombinu, kuongeza ajira, kuvutia uwekezaji na kuifanya Sinza kuwa eneo la kisasa lenye ushindani mkubwa wa kiuchumi.

Amesisitiza kuwa, utekelezaji wa mpango huo utaongozwa na sheria, sera na taratibu za nchi huku haki za wamiliki wa ardhi zikiheshimiwa kikamilifu.

"Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wa Sinza wanakuwa washiriki, wabia na wanufaika wakuu wa maendeleo yatakayozalishwa na Mpango huu, badala ya kuwa watazamaji wa maendeleo hayo." amesema

Kwa mujibu wa Dkt Akwilapo, mpango huo umekuwa ukitumika katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kuendeleza maeneo ya mijini yaliyopangwa kwa viwanja vidogo vidogo na umeonyesha mafanikio katika kuboresha matumizi ya ardhi na huduma za kijamii.

Kupitia mpango huo, wamiliki wa ardhi wataendelea kuwa sehemu ya maendeleo ya maeneo yao kwa kuchangia ardhi kwa pamoja ili kuwezesha upatikanaji wa miundombinu, huduma za jamii na maeneo ya maegesho, huku wakiendelea kunufaika na ongezeko la thamani ya ardhi na mali zao baada ya utekelezaji wa mpango.

“Lengo la Serikali si kuchukua ardhi za wananchi, bali kuweka mazingira yatakayowezesha matumizi bora zaidi ya ardhi, kuongeza thamani ya mali za wananchi, kuboresha ubora wa makazi na kuimarisha fursa za kiuchumi,” amesema.

Aidha, Serikali imeahidi kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mpango huo unazingatia kikamilifu haki za wamiliki wa ardhi, ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi, uwazi katika mchakato wa utekelezaji pamoja na uzingatiaji wa sheria, sera na taratibu zote za nchi.

Ametoa rai kwa wananchi wote kuwa waangalifu dhidi ya watu wanaoweza kutumia taarifa za Mpango huu kwa maslahi binafsi kwa kuwashawishi muuze ardhi zenu kwa bei zisizoendana na thamani yake ya baadaye.

‘’Ni muhimu kutambua kuwa eneo la Sinza linaendelea kuwa mojawapo ya maeneo yenye mvuto mkubwa wa uwekezaji katika Jiji la Dar es Salaam. Hivyo, wananchi wanapaswa kufanya maamuzi kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia maslahi yao ya muda mrefu’’. amesema

Kwa upande wake Waziri Nchi Ofisi ya Raisi Mipango na Uwekezaji ambaye ni mbunge wa jimbo la Ubungo Profesa Kitila Mkumbo amesema, zoezi hilo lipo kwa nia njema ya maendeleo ya wananchi wa Sinza na kusisitiza zoezi hilo kufanyika kwa haraka haraka.

‘’Serikali haiwezi kuchukua hatua zozote za kuharibu maisha ya wananchi wake lengo la serikali ni kujenga ustawi wa watu wake’’ amesema Prof Kitila Mkumbo

Naye Meya wa Manispaa ya Ubungo Mhe. Lawrence Mlaki amesema kata ya Sinza ni moja ya kata 14 zilizopo kwenye manispaa yake na hali ya eneo hilo imebadilika sana kutokana na ujenzi wa maghorofa na maduka hivyo ipo haja ya kufanyiwa mabadiliko na mpango wa kuiboresha upya Sinza umekuja wakati muafaka.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akifungua mkutano wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu rasimu ya mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Katikati), Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo (Kulia) na Naibu Waziri wa Ardhi Kaspar Mmuya (Kushoto) wakibadilishana mawazo wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu rasimu ya mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Kushoto) akisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu rasimu ya mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026.

Sehemu ya washiriki wa mkutano wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu rasimu ya mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera (Katikati) akifuatilia uwasilishaji wa rasimu ya mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026. Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Bw. Deogratius Kalimenze.Mbunifu Majengo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Arch. Tutindaga Jacobs akiwasilisha mpango wa muonekano mpya wa Sinza wakati wa uwasilishaji wa rasimu ya mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026. Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Deogratius Kalimenze.
Mmoja wa wadau kutoka eneo la Sinza akitoa maoni yake kuhusiana na mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 6 Juni 2026. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)



No comments: