Mchengerwa: Afrika haitaweza kujenga uchumi kwa mzigo wa magonjwa yasiyotibiwa

 

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwa  niaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifungua mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa kikanda wa Pen-Plus kuhusu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza makali (ICPPA 2026) unaofanyika kwa siku gatu kuanzia leo Juni 23, 2026 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa JNICC, jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya afrika, Profesa Mohamed Janabi akizungumza  wakati ufunguzi wa mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa kikanda wa Pen-Plus kuhusu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza makali (ICPPA 2026) unaofanyika kwa siku gatu kuanzia leo Juni 23, 2026 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa JNICC, jijini Dar es Salaam
Ofisa Programu wa PEN-Plus kutoka Helmsley Charitable Trust,  James Reid  akizungumza wakati ufunguzi wa mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa kikanda wa Pen-Plus kuhusu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza makali (ICPPA 2026) unaofanyika kwa siku gatu kuanzia leo Juni 23, 2026 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa JNICC, jijini Dar es Salaam




Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika linatishia maendeleo ya kijamii na kiuchumi, akisisitiza kuwa bara hilo haliwezi kujenga uchumi imara huku likiendelea kubeba mzigo wa magonjwa ambayo hayapati matibabu kwa wakati.

Mchengerwa amesema hayo kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Kimkakati wa kikanda wa Pen-Plus kuhusu kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza makali (ICPPA 2026) leo Juni 23, 2026 jijini Dar es Salaam

Amesema magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya moyo na selimundu yanaongezeka kwa kasi na kuathiri uzalishaji pamoja na ustawi wa familia.

kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza husababisha zaidi ya vifo milioni 43 duniani kila mwaka, sawa na asilimia 74 ya vifo vyote.

Hivyo, Mchengerwa amesema Tanzania imeongeza uwekezaji katika kukabiliana na magonjwa hayo kwa kuongeza bajeti ya huduma husika kutoka asilimia saba ya matumizi ya afya mwaka 2020 hadi zaidi ya asilimia 24 mwaka 2024, sambamba na kuboresha vifaa vya uchunguzi na matibabu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, amesema magonjwa yasiyoambukiza si tishio la baadaye bali ni changamoto ya sasa inayohitaji hatua za haraka za kuimarisha kinga, uchunguzi wa mapema na huduma za afya ya msingi.

Amesema wagonjwa wengi barani Afrika bado hugundulika katika hatua za mwisho za ugonjwa, hali inayochangia kuongezeka kwa vifo na gharama kubwa za matibabu kwa familia na serikali.

Amesisitiza kuwa kuwekeza katika kinga na uchunguzi wa mapema ni hatua muhimu katika kupunguza mzigo wa magonjwa hayo.

Profesa Janabi pia aliipongeza Tanzania kwa mafanikio yake katika sekta ya afya, ikiwemo kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya wajawazito, hatua aliyosema imeokoa maisha ya maelfu ya wanawake na kuziwezesha familia nyingi kuendelea kuwa pamoja.

Pia, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambuliwa kama Bingwa wa Afya ya Mama Barani Afrika, akisema mafanikio hayo yanaonyesha dhamira ya uongozi wa Tanzania katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa wananchi.

Naye Ofisa Programu wa PEN-Plus kutoka Helmsley Charitable Trust, James Reid, amesema zaidi ya wagonjwa 170,000 katika nchi 20 za Afrika tayari wamenufaika na huduma zinazotolewa kupitia mpango huo, ambao unalenga kusogeza huduma za magonjwa sugu karibu na wananchi.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika nchi mbalimbali yanaonyesha umuhimu wa serikali kuendelea kuwekeza katika mifumo ya afya na kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Reid ameongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali, wadau wa maendeleo na taasisi za afya ni muhimu katika kupanua huduma za PEN-Plus na kuhakikisha watu wengi zaidi wenye magonjwa sugu wanapata matibabu kwa wakati.

No comments: