SERIKALI YAISIFU CRDB KWA KUKUZA UWEKEZAJI WA VIJANA



Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Serikali imeipongeza Benki ya CRDB Bank Plc kwa juhudi zake za kuhamasisha uwekezaji nchini kupitia elimu ya fedha, uwekezaji wa hisa na uwezeshaji wa kiuchumi unaolenga kuwajenga vijana kuwa wawekezaji wa baadaye.

Pongezi hizo zimetolewa jana jijini Arusha na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa 31 wa mwaka wa benki hiyo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).

Semina hiyo ilikuwa na kaulimbiu isemayo “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa” na iliwakutanisha viongozi wa serikali, wanahisa, wataalamu wa masoko ya mitaji pamoja na vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza katika semina hiyo, Waziri Omar alisema vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika umiliki wa uchumi kupitia uwekezaji badala ya kutegemea ajira pekee.

“Kaulimbiu ya mwaka huu imebeba ujumbe mkubwa wa kimkakati kwa taifa letu. Vijana hawapaswi kuishia kutafuta ajira pekee, bali wanastahili kushiriki katika umiliki wa uchumi kupitia uwekezaji,” alisema Waziri Omar.

Aidha, aliipongeza benki hiyo kwa hatua ya kufungua Ofisi ya Uwakilishi Dubai, akisema hatua hiyo imeongeza hadhi ya Tanzania katika sekta ya fedha na uwekezaji kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo itaendelea kuwawezesha vijana kupitia huduma za kifedha, ubunifu na programu za maendeleo ya ujasiriamali.

Alisema kupitia CRDB Bank Foundation na programu ya IMBEJU, maelfu ya vijana na wafanyabiashara wadogo wamefikiwa kwa mafunzo, mitaji na ushauri wa biashara.

“Tunaamini vijana wa leo si wateja tu wa benki yetu, bali ni wawekezaji, wabunifu na viongozi wa uchumi wa kesho,” alisema Dkt. Nsekela.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Neema Mori alisema uwekezaji katika hisa ni njia muhimu ya kujenga ustawi wa kifedha wa muda mrefu kwa vijana na familia za Kitanzania.

Profesa Mori alisema mafanikio ya Benki ya CRDB yanaonyesha namna uwekezaji wa muda mrefu unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa wanahisa.

Alibainisha kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita thamani ya hisa za benki hiyo imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 253, huku bei ya hisa ikifikia wastani wa Sh2,800 kutoka Sh460 mwaka 2023.

Aidha, alisema bodi ya wakurugenzi inapendekeza gawio la Sh90 kwa kila hisa kutokana na matokeo mazuri ya kifedha ya mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Profesa Mori aliwahamasisha wazazi kuanza kuwawekezea watoto wao hisa mapema ili kuwajengea msingi imara wa maisha ya kifedha ya baadaye.

Benki ya CRDB ni miongoni mwa taasisi kubwa za kifedha Afrika Mashariki na Kati, ikiwa na zaidi ya wateja milioni sita katika nchi za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na ofisi ya uwakilishi Dubai, Falme za Kiarabu.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati akifungua Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa, uliobeba kauli mbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa”, semina inayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), ambapo alitoa wito kwa Taasisi za Fedha nchini kupunguza riba na gharama nyingine za mikopo ili kuwawezesha wananchi wakiwemo vijana kupata mitaji ya kuwekeza kwenye shughuli zao za kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa hao, uliobeba kauli mbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa”, uliofunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Prof. Neema Mori, akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB katika Mkutano Mkuu wa 31 wa Wanahisa hao, uliobeba kauli mbiu ya “Vijana na Uwekezaji kwenye Hisa”, uliofunguliwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC).









No comments: