Serikali Kuajiri Watumishi 45,000 Mwaka 2026/27
Kuwabadilishia muundo watumishi 5,865, kuwapandisha madaraja watumishi 234,921.
Na. Jawadu Kinyobwa - Arusha
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhururi ya Muungano wa Tanzania imepanga kuajiri watumishi wapya 45,000 wa kada mbalimbali katika mwaka wa fedha 2026/27 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha utumishi wa umma na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma nchini.
Mbali na ajira hizo mpya, Serikali pia imepanga kuwabadilishia muundo watumishi 5,865 pamoja na kuwapandisha madaraja watumishi 234,921.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 21, 2026 na Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha Menejimenti ya Waandishi Waendesha Ofisi (TAPSEA) uliofanyika Ngurdoto, jijini Arusha.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira bora na wezeshi ya kazi kwa watumishi wa umma ili kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi.
Amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 Serikali imeidhinisha ajira mpya za watumishi 42,500 wa kada mbalimbali, kupandisha vyeo watumishi 219,042, kuwabadilishia muundo watumishi 6,198 pamoja na kulipa malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 18,083.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ridhiwani amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii na weledi huku akiwaasa waajiri kusimamia ipasavyo utendaji kazi wa watumishi ili kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
No comments: