SAMIA, KAGAME WAWEKA MKAZO BIASHARA, UWEKEZAJI NA MIUNDOMBINU KUIMARISHA UCHUMI WA KIKANDA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Ziara ya Kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Mei, 2026
Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Rwanda zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kwa kuondoa vikwazo vya biashara na kuvutia uwekezaji zaidi ili kukuza uchumi wa nchi hizo mbili na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Rais Samia ameyasema hayo May 3,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda Paul Kagame katika ziara yake nchini.
Rais Samia alisema uhusiano wa Tanzania na Rwanda ni wa kihistoria, unaotokana na undugu, urafiki na kufanana kwa tamaduni, mila na desturi za wananchi wake.
Alieleza kuwa kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC), nchi hizo zimeendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, uwekezaji, kilimo, nishati, miundombinu ya usafiri, ulinzi, usalama pamoja na masuala ya uhamiaji.
Amebainisha kuwa biashara kati ya Tanzania na Rwanda imefikia thamani ya shilingi bilioni 644 mwaka jana, huku uwekezaji kutoka Rwanda nchini ukifikia miradi 42 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 325.5 iliyozalisha ajira 2,225 kwa Watanzania.
Aidha, alisema licha ya mafanikio hayo, bado kuna umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi ili kurahisisha biashara na kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Soko Huria la Afrika (AfCFTA).
Katika sekta ya miundombinu, Rais Samia alisema takribani asilimia 70 ya mizigo ya Rwanda hupitia bandari za Tanzania, hivyo kuna haja ya kuboresha zaidi huduma za usafirishaji ikiwemo reli ya Isaka hadi Kigali pamoja na barabara zinazounganisha nchi hizo ili kuongeza ufanisi wa biashara.
Aligusia pia ushirikiano wa nishati akitaja mradi wa umeme wa maji wa Rusumo wenye uwezo wa megawati 80 pamoja na makubaliano ya biashara ya umeme kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Rwanda (REG), hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya viwanda na uchumi.
Kwa upande wake, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, alisema ushirikiano huo ni nguzo muhimu ya maendeleo ya mataifa hayo na ukanda mzima, akisisitiza kuwa mazungumzo yao yamelenga zaidi kuimarisha biashara, uwekezaji na miundombinu.
Rais Kagame alitambua mchango wa Tanzania katika kuhudumia biashara ya Rwanda kupitia bandari zake na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza na kuboresha huduma hizo ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa.
Aidha, alisisitiza haja ya kuondoa vikwazo vya kibiashara vinavyokwamisha ukuaji wa uchumi na kuhimiza matumizi bora ya fursa zilizopo katika masoko ya kikanda na bara la Afrika.
Katika sekta ya nishati na mawasiliano, Rais Kagame alisema ushirikiano uliopo, ikiwemo miradi ya pamoja na matumizi ya miundombinu ya mawasiliano, utaendelea kuimarishwa ili kusaidia ukuaji wa uchumi na uwekezaji.
Viongozi hao wawili pia walisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, usalama na utulivu kama msingi wa maendeleo endelevu, huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano wa karibu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania, Rwanda na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.

Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame akizungumza na Waandishi wa Habari kufuatia Ziara yake ya Kikazi Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Mei, 2026
Matukio mbalimbali katika Ziara ya Kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame, Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 03 Mei, 2026.





No comments: