Benki ya Absa Tanzania Yazindua huduma ya mikopo isiyo na dhamana ili kukuza biashara za wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Benki ya Absa Tanzania imezindua rasmi suluhisho bunifu la mikopo ya muda mfupi inayolenga kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati kukuza biashara zao bila hitaji la dhamana.

Huduma hiyo mpya imeundwa mahsusi kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya bidhaa na huduma, wakiwemo wauzaji wa jumla, wasambazaji, mawakala na wauzaji wa rejareja wanaotumia mashine za malipo zinazotolewa na benki hiyo, Absa Point-of-Sale (POS) pamoja na njia nyingine za kidijitali za malipo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Njia za Malipo wa Benki ya Absa Tanzania, Jane Kalumuna, alisema huduma hiyo inalenga kuondoa changamoto kubwa inayowakabili wafanyabiashara wengi ya kushindwa kupata mikopo kutokana na kukosa dhamana za kawaida.

Alisema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakifanya mauzo ya kila siku yenye mtiririko mzuri wa fedha, lakini bado wamekuwa wakikosa fursa za kupata mikopo kwa sababu mifumo mingi ya kifedha hutegemea zaidi dhamana kuliko uwezo halisi wa biashara.

“Kwa muda mrefu, biashara nyingi zenye mtiririko mzuri wa fedha zimekuwa zikikosa huduma za kifedha kwa sababu hazina dhamana za kawaida. Kupitia Absa huduma hii, tunabadilisha simulizi hilo kwa kutambua na kuthamini utendaji halisi wa biashara,” alisema Bi. Jane.

Aliongeza kuwa huduma hiyo inatumia historia ya miamala ya POS kupima uwezo wa mfanyabiashara kukopa, hivyo kuwezesha wafanyabiashara kupata fedha kwa haraka kulingana na mwenendo halisi wa biashara zao.

Naye Meneja Masoko na Mawasiliano na Chapa wa Benki ya Absa Tanzania, Beda Biswalo, alisema huduma hiyo ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo ya kuwezesha ukuaji wa biashara na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.

“Kwa kuondoa kikwazo cha dhamana na kubadilisha mauzo ya kila siku kupitia POS kuwa chanzo cha haraka cha mtaji, tunabadilisha namna biashara zinavyopata huduma za kifedha nchini Tanzania. Tunaamini kuwa kila mfanyabiashara ana simulizi muhimu, na suluhisho hili linaakisi ahadi yetu ya kusikiliza na kusaidia ukuaji wao,” alisema Biswalo.

Aliongeza kuwa kupitia huduma hiyo, Absa inaendeleza dhamira yake ya ‘Kuiwezesha Afrika ya Kesho Pamoja, Hatua Moja baada ya Nyingine’ kwa kusaidia biashara kukua, kupanuka na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Huduma ya Absa Merchant Financing inatarajiwa kusaidia kuziba pengo la upatikanaji wa mikopo kwa wafanyabiashara wengi nchini huku ikiimarisha ujumuishaji wa kifedha na mahusiano ya muda mrefu kati ya benki na wateja wake.


 Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Njia za Malipo wa Benki ya Absa Tanzania, Jane Kalumuna (wa tatu kushoto) na wengine kutoka kushoto; Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa, Beda Biswalo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na wa Kati, Scolastica Dominic na Meneja Mauzo wa Kitengo cha machine za malipo (POS), Edward Edwine, wakionesha mashine hizo kama ishara ya uzinduzi rasmi wa huduma ya mikopo isiyo na dhamana yenye lengo la kukuza biashara za wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaofanya mauzo kwa kutumia POS za Absa. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo.


Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Njia za Malipo wa Benki ya Absa Tanzania, Jane Kalumuna (wa tatu kushoto) na wengine kutoka kushoto; Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa, Beda Biswalo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na wa Kati, Scolastica Dominic na Meneja Mauzo wa Kitengo cha machine za manunuzi (POS), Edward Edwine, wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari, jijini Dar es leo, katika hafla ya uzinduzi rasmi wa huduma ya mikopo isiyo na dhamana yenye lengo la kukuza biashara za wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaofanya mauzo kwa kutumia POS za Absa.
Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa na Njia za Malipo wa Benki ya Absa Tanzania, Jane Kalumuna (wa tatu kushoto, waliokaa) na wengine kutoka kushoto; Meneja Masoko, Mawasiliano na Chapa, Beda Biswalo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na wa Kati, Scolastica Dominic na Meneja Mauzo wa Kitengo cha machine za manunuzi (POS), Edward Edwine, wakionesha mashine hizo kama ishara ya uzinduzi rasmi wa huduma ya mikopo isiyo na dhamana yenye lengo la kukuza biashara za wafanyabiashara wadogo na wa kati wanaofanya mauzo kwa kutumia POS za Absa. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam leo. Wengine ni baadhi ya wafanyakazi wa kitengo cha biashara.



No comments: