NAIBU WAZIRI WA FEDHA AFUNGUA MKUTANO WA NNE WA WAKAGUZI WA NDANI

 


Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Nne wa Wakaguzi wa ndani wa Taasisi na sekta za umma, ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa ndani nchini Tanzania (IIA), Mkoani Morogoro.

Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani, Bw. Jonathan Ngoma akizungumza katika Mkutano wa Nne wa Wakaguzi wa ndani wa Taasisi na sekta za umma, ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa ndani nchini Tanzania (IIA), Mkoani Morogoro.

Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Nne wa Wakaguzi wa ndani wa Taasisi na sekta za umma, ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa ndani nchini Tanzania (IIA), Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula akifungua Mkutano wa Nne wa Wakaguzi wa ndani wa Taasisi na sekta za umma, ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa ndani nchini Tanzania (IIA), Mkoani Morogoro.




Na Mwandishi Wetu, Morogoro

NAIBU Waziri wa Fedha, Bw. Laurent Luswetula amewataka wakaguzi wa Ndani wa taasisi na sekta za umma nchini kuongeza ufanisi kwa kazi zao na kuhakikisha wanakuwa huru ili fedha na rasilimali zinazotolewa na Serikali kwa jamii zitumike kama zilivyo tarajiwa.

Bw. Luswetula ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa nne wa wakaguzi wa ndani wa Taasisi na sekta za umma, ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa ndani nchini Tanzania (IIA), ambapo alisisitiza wakaguzi hao kuwa huru kwa kuwa wao ndio macho ya Serikali katika matumizi ya fedha kwa mashirika ya umma na miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

"Hawa wakaguzi ndio hutoa taswira ya namna ya fedha iliyoidhinishwa na kutolewa na Serikali kama imefika kwenye miradi au taasisi na pia wanaangalia kama fedha hizo zimetumika kwa usahihi," alisema Naibu Waziri Luswetula.

Alibainisha kuwa jukumu mojawapo la wakaguzi hao ni kuwa tayari kuhakikisha kwamba wanachunguza na kutoa majawabu sahihi kwa maana ya kutomuonea wala kumpendelea mtu yeyote.

Aidha aliongeza kuwa Serikali ipo tayari kuwaunga mkono wakaguzi katika kazi zao kuhakikisha wanafanyakazi katika mazingira yenye uhuru na yasiyo na vitisho na endapo patatokea muingiliano kwenye majukumu yao wawe huru kutoa taarifa hiyo mapema ili ufumbuzi upatikane.

Naye Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani, Bw. Jonathan Ngoma akizungumza katika mkutano huo aliainisha kukosekana kwa uhuru kwa baadhi ya wakaguzi ndiko kunakosababisha kuendelea kwa mapungufu ya kiutendaji katika kaguzi kadhaa zinazofanyika maeneo mbalimbali.

"Mkaguzi yeyote anatakiwa awe huru aseme hapa kuna matatizo lakini sasa usipokuwa huru hutaweza kuyasema matatizo unayoyaona na ndio maana tumekuwa na matatizo ambayo hayaishi,...mwingine anayaona halafu wewe huyaoni na wakati mwingine hata akiyaona ataambiwa liache kama lilivyo, matokeo yake tunaishia mahali ambapo matatizo yataendelea kuwepo," alisema Bw. Ngoma.

Naye Msajili wa Hazina Zanzibar Waheed Muhammad Ibrahim amesema mafunzo hayo yanawajengea uwezo wa kuzitambua mbinu za ukaguzi zitakazowasaidia kwenye kazi zao za ukaguzi, huku Mkaguzi Mkuu wa Ndani Soko la hisa la Dar es salaam, Bw. Mecklaud Edson akisisitiza wakaguzi wa ndani kuwa macho ya serikali katika matumizi ya fedha kwa mashirika ya umma na miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, alisema masuala ya kiutawala yanapaswa kupewa kipaumbele na kuwekewa mkazo katika taasisi za umma hasa zile zinazohusika katika masuala ya uwekezaji moja kwa moja pamoja na zenye bodi za wakurugenzi ili kuleta chachu na hatimaye kufikia malengo ya taasisi.

Mkutano wa nne wa Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani na sekta za umma umewakutanisha wakaguzi wa ndani kutoka Taasisi mbalimbali za umma kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo na kuzisaidia kamati za ukaguzi za ndani kutenda kazi zao vyema na ufanisi, kuweza kuhoji utawala kuhoji wakaguzi wa ndani na vitengo vya ukaguzi ili kuboresha huduma kwa wateja na watanzania wanaohitaji huduma.





No comments: