TUME YA MADINI YAFUNGUA FURSA KWA VIJANA
Na Mwandishi wetu - Dodoma.
Tume ya Madini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wachimbaji hasa vijana katika eneo la uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani pamoja na biashara ya Madini.
Katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2025 Tume ya Madini imehakikisha inatekeleza Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania ili kuongeza Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya madini. Migodi ilifanya manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kampuni za Watanzania zikiwemo za vijana na zilizoajiri vijana yenye thamani ya Shilingi Trilioni 3.8.
Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Madini Mhandisi Hamis Kamando ameyabainisha hayo leo jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari wakati akitangaza miradi ya maendeleo na fursa za vijana kwa mwaka 2025/26, ambapo amesema Tume ya Madini kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa STAMICO na kituo cha Jemolojia cha Tanzania, imeendelea kutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wachimbaji hasa vijana.
Vilevile, Tume ya Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini (Upskills Program) ilitoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo 579.
Pia Tume ya Madini imeingia makubaliano na Benki ya CRDB ili kuanza utekelezaji wa mpango wa kutoa mitaji kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu hasa vijana. Hati ya Makubaliano hayo imesainiwa tarehe 23 Februari, 2026.
Mhandisi Kamando amesema miongoni mwa maeneo ambayo Tume ya Madini inatarajia kuyatilia mkazo katika kipindi cha Mwaka 2026/2027 kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa kundi la vijana ni pamoja na ujenzi wa majengo ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi, uendelezaji wa minada na maonesho ya ndani ya madini ya vito, kutenga maeneo zaidi kwa vijana kila mkoa, na kushirikiana na Taasisi za kifedha katika kuangalia namna bora ya upatikanaji wa mitaji kwa vijana.
Pia Tume ya Madini imendelea kushirikiana na kundi la vijana katika kuhakikisha rasilimali iliyopo inawanufaisha ipasavyo pamoja na Taifa kwa ujumla. Dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha rasilimali hii inawanufaisha vijana wasasa pamoja na vizazi vijavyo.




No comments: