Angellah Kairuki: Wanahabari Wanawake Ni Nguzo Muhimu Kutatua Changamoto za Jamii

 



Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema mchango wa wanahabari wanawake ni mkubwa katika kutatua changamoto mbalimbali za jamii, zikiwemo za kijamii na kiuchumi zinazowakabili wanawake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Malkia wa Habari lililoandaliwa na waandishi wa habari wanawake, Kairuki alisema wanahabari wanawake wanapaswa kutumia vyema kalamu zao kama daraja la kuwasilisha changamoto za wananchi kwa serikali ili kupatiwa ufumbuzi.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amewataka waandishi hao kusimamia kikamilifu vikundi na vyama wanavyoanzisha, sambamba na kuhakikisha vinazalisha matokeo chanya kwa wanachama na jamii kwa ujumla.

Aidha, alibainisha kuwa kuna fursa nyingi katika tasnia ya habari na mawasiliano, hivyo wanawake wanapaswa kuzichangamkia ipasavyo, akisisitiza kuwa serikali ipo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika.

Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wanahabari wanawake waliopata ithibati kuwa na umoja, hatua itakayorahisisha utambuzi wao rasmi na serikali.

Kwa upande wake, Mratibu wa kongamano hilo, Penina Malundo, alisema lengo la mkutano huo ni kujadili changamoto zinazowakabili wanahabari wanawake, kuimarisha ushirikiano wao katika shughuli za kijamii, na kusaidia kuinua sauti ya wanawake katika vyombo vya habari.

Naye Mhariri wa Habari za Siasa wa gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka, aliwataka wanahabari wanawake kujitokeza kutafuta maarifa na kujifunza kwa bidii badala ya kusubiri mafunzo rasmi.

Kwa upande mwingine, Mhariri Mkuu wa Clouds Media, Joyce Shebe, aliwahimiza wanawake kutafuta mbinu mbalimbali za kukabiliana na taarifa hasi zinazosambaa mitandaoni.

Aidha, Mhariri wa Habari wa gazeti la Tanzania Leo, Marry Geofrey, alisema kongamano hilo limewapa fursa wanahabari wanawake kujieleza na kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili katika kazi zao za kila siku.

No comments: