WAZIRI DK. HOMERA KUONGOZA UTOAJI WA MSAADA WA KISHERIA MOROGORO
*Huduma za haki kwa wananchi zatolewa kesho kupitia kliniki za msaada wa kisheria na ziara ya kikazi ya Wizara
Na Mwandishi Wetu
KUELEKEA siku 100 za Rais Ikulu, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, anatarajiwa kuongoza zoezi la utoaji wa msaada wa kisheria bure mkoani Morogoro kesho, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mapema wa vipaumbele vya Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Kwa mujibu wa bango la taarifa ya Wizara, wananchi wenye changamoto mbalimbali za kisheria wanakaribishwa kujitokeza kupata huduma hizo, hususan wanaokabiliwa na migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, malezi na ulinzi wa watoto, vyeti vya kuzaliwa, pamoja na changamoto nyingine zote zinazowatatiza wananchi na kuhitaji ufumbuzi wa kisheria.
Huduma hiyo itatolewa kupitia kliniki maalum za msaada wa kisheria zitakazowahusisha wataalamu wa sheria na taasisi zilizo chini ya Wizara, ambapo wananchi watapata elimu ya kisheria, ushauri wa kitaalamu na mwongozo wa hatua za kuchukua kulingana na changamoto zao.
Aidha, mkutano maalum wa kusikiliza na kutatua changamoto hizo kwa pamoja unatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Stendi ya Zamani, Morogoro, ambapo wananchi watapata fursa ya kuwasilisha kero na hoja zao moja kwa moja kwa wataalamu wa sheria na viongozi wa taasisi husika.
Mbali na utoaji wa huduma hizo, Waziri anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika taasisi za haki zilizopo mkoani humo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu, kusikiliza changamoto na kutoa maelekezo yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za kisheria kwa wananchi.
Hatua hii inalenga kuisogeza huduma ya haki karibu na wananchi, hususan makundi yenye uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria, sambamba na mkazo wa Serikali wa kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati, kwa usawa na bila vikwazo.
Ziara hii ya Morogoro ni sehemu ya mwendelezo wa shughuli za Wizara ya Katiba na Sheria katika kuimarisha utawala wa sheria nchini, na inaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma za kisheria zinawafikia wananchi moja kwa moja walipo.

No comments: