Nsekela apokoea maelekezo ya Serikali kuifufua sekta ya chai

====== =======
Dodoma. Tarehe 8 Aprili 2025: Katika mkakati wa kuongeza mchango wa sekta ya chai nchini, serikali imemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania (TBT) ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB pia, Abdulmajid Nsekela kuhakikisha anatumia uzoefu wake katika sekta ya fedha pamoja na uzoefu walionao wajumbe wake kushughukia changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo ya chai nchini.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe alipozindua bodi mpya ya wakurugenzi ya TBT kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wadau wa tasnia ya chainchini uliofanyika jijini hapa.
Bashe amesema tangu awe waziri wa kilimo haridhishwi na maendeleo yaliyopo kwenye zao la chai kutokana na mambo mengi yanayoendelea ikiwamo kushuka kwa mapato yatokanayo na mauzo yake nje ya nchi, wasafirishaji kutoelewa kwa uwazi kiasi wanachokipeleka nje ya nchi na kushuka kwa kiasi kinachozalishwa nchini kilamwaka.
“Tulipokuwa tunatafuta mwenyekiti mpya wa Bodi ya Chai Tanzania tulisema tumpate mtu anayetoka sekta ya fedha atakayeijua sekta ya chai ambayo changamoto yake kubwa ni upatikanaji wa mikopo ili ashiriki kuitatua changamoto hiyo na kuifanya sekta hii ikue na kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye kipato cha wakulima na wadau wa sekta ya chai pamoja na kuchangia zaidi kwenye pato la taifa,” amesema Mheshimiwa Bashe.
Baada ya kumpata mwenyekiti, amesema waliwatafuta wajumbe wenye ujuzi na uzoefu katika sekta tofauti ikiwamo masoko ili wasaidie kuweka mkakati wa kuitengenezea nembo imara chai ya Tanzania itakayoiwezesha kushindana kimataifa.
Kwenye maelekezo yake kwa bodi hiyo ya wakurugenzi pamoja na menejimenti ya TBT, Waziri Bashe amesema changamoto zote zilizopo kwenye sekta ya chai ni mfumo wake hivyo ameitaka bodi ya wakurugenzi kuupitia mpango mkakati waTBT pamoja na sera ya chai na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuziondoa kero zilizopo.
“Hakikisheni kunakuwa na uwazi wa taarifa kwa sababu wapo baadhi ya wasafirishaji ambao hawaisajili mikataba yao yote hivyo kuinyima serikali taarifa sahihi. Kwa msafirishaji atakayebainika kutotoa taarifa za mzigo anaosafirisha afutiwe leseni. Sekta ya chai inao wadau wasiopenda kukutana, kila mmoja anataka afanye mambo yake kivyake. Undeni kamati itakayowahusisha wadau wengine kuangali namna ya kuyashughulikia matatizo tuliyonayo ili tuwe na chai bora zaidi,” amesisitiza Waziri Bashe.
Akionyesha utayari wa kuyatekeleza maelekezo hayo, Nsekela aliyeteuliwa Februari 2025 kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TBT amesema anayo imani watazishughulikia kero zilizopo na kuifanya sekta ya chai kuwa na mchango mkubwa zaidi kuanzia kwa wakulima mpaka viwanda vinavyolichakata zao hilo.
“Tunahitajia maridhiano kwa kuwajumuisha wadau wote katika sekta ya chai. Asiwepo anayefaidi zaidi ya mwenzake. Ni lazima tufanye mabadiliko ya uwazi. Kila mdau awe na atoe taarifasahihi. Katika hatua hizo zote, tutahitaji ustahimilivu wa kuleta maboresho tunayoyakusudia. Tutafanya marekebisho muhimu katika mnyororo mzima wa zao la chai na tukisikilizana, tutafanikiwa kujenga pamoja,” amesema Nsekela akizinukuu 4R za Rais Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kwamba zikitumika katika maeneo tofauti zinaweza kubadili hali iliyopo na kuleta maisha bora kwa Watanzania.
Licha ya uzoefu wake mkubwa katika sekta ya fedha nchini, Nsekela pia anaifahamu sekta ya kilimo kwani alikuwamwenyekiti wa Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHTDA) kabla haujaunganishwa na TBT hivi karibuni na ni mwenyekiti wa Kamisheni ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania.
Tanzania kuna zaidi ya wakulima wadogo 32,000 wa chai huku wananchi wengine zaidi ya milioni 2 wakipata ajira zisizo za moja kwa moja katika sekta hii.
Kuanzia Disemba 2024 hadi Machi 2025, Tanzania imeingiza zaidi ya Shilingi bilioni 50.25kutokana na vibali vya kusafirisha chai nje ya nchi vinavyotolewa na TBT.
Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali imewavutia wawekezaji waliowekeza katika maeneo ya Kilolo, Njombe na Mbeya.Aidha, wawekezaji na wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani wameendelea kujitokeza ili kuwekeza na kununua chai ya Tanzania.
Akizungumzia baadhi ya kero zilizopo, Mwenyekiti wa Wakuu wa Wilaya kutoka halmashauri zinazolima chai nchini, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Mheshimiwa Jaffer Haniu ameitaja bei ndogo ya majani mabichi ya chai na kuchelewa kwa malipo ya wakulima pamoja na kufungwa kwa viwanda vya chai kuwa kunawakatisha tamaa wakulima.
No comments: