Rais wa TWCC Atoa Wito kwa Wanawake na Vijana Wafanyabiashara Kushirikiana Katika Biashara
Rais wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya uwezeshaji wa Wanawake na Vijana kushiriki katika manunuzi ya umma. Mafunzo hayo yanafanyika jijini Dar es Salaam leo Machi, 06, 2025.
Baadhi ya Wanawake na Vijana wakiwa kwenye mafunzo kuwawezesha manunuzi ya umma.
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
RAIS wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza, ametoa wito kwa wanawake na vijana wafanyabiashara kushirikiana na kupeana kazi pale wanapopata tenda za kufanya.
Hayo ameyasema leo Machi 6, 2025 jijini Dar es Salaam, Akifungua mafunzo ya uwezeshaji wa wanawake na vijana kushiriki katika manunuzi ya umma, Rais Hamza alisema kuwa ushirikiano ni muhimu kwa kuhakikisha mafanikio katika sekta ya biashara.
Amewasisitizia washiriki wa mafunzo kuepuka tabia ya kuomba tenda au zabuni mara mbili kwa kutumia kampuni tofauti, akisema kuwa hatua hiyo ni kinyume na maadili ya uombaji wa zabuni na inaweza kuharibu uaminifu na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara au kufungiwa kuomba tena.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika kwa miezi sita mfululizo kila mwaka kuanzia 2024 hadi 2026, ambapo yatatoa fursa kwa washiriki kujifunza ujuzi wa kuomba na kuandika tenda. Mafunzo haya pia yatasaidia vijana na wanawake wafanyabiashara kuongeza ufanisi wao katika kushiriki kwenye masoko ya manunuzi ya umma.
Aidha, Rais wa TWCC amewataka wafanyabiashara kutembelea mtandao wa NeSt (National e-Procurement System), ambao unatoa taarifa muhimu kuhusu tenda zinazotangazwa na serikali pamoja na kutembelea mitandao mingine inayotangazaa tenda na zabuni mbalimbali ili kuchangamkia fursa zinazotolewa.
Ameeleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi zilizojiunga na uwanachama wa nchi zinazotangaza tenda katika masoko ya kimataifa kama vile soko la bara la Afrika, SADC, UN, na Soko la Afrika Mashariki, na kwamba wafanyabiashara wa Kitanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa za kuomba tenda zinazotangazwa na nchi hizo.
“Hakuna mchawi katika kufanya kazi vizuri na kwa uaminifu, pesa utapata,” amesema Rais Hamza.
Ameongeza kuwa, watu wengi wanapewa kazi lakini wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa viwango vinavyohitajika, jambo linalosababisha kushindwa kwa miradi na kupungua kwa uaminifu katika biashara.
Lengo la TWCC, amesema ni kuandaa programu hii kwa ajili ya kuwasaidia vijana, hasa katika kujua jinsi ya kuomba tenda, kuandika tenda, na kukuza kampuni zao. Alihimiza kuwa kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa viwango bora, vijana wataweza kupata fedha na kufanikiwa katika biashara zao.
Mafunzo haya ya kipekee yanatoa fursa kwa wanawake na vijana wafanyabiashara kuwa na ufanisi mkubwa katika sekta ya manunuzi na biashara, huku wakijengewa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika masoko ya kimataifa.
Picha za pamoja.
No comments: