NMB WACHANGIA SHULE NA ZAHANATI MKURANGA



Na Khadija Kalili, Michuzi TV
KATIKA kushehereke maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani Benki ya NMB imesherehekea kwa kutoa msaada wa madawati 100 na vitanda 20 kwa Shule mabati 100 kwa ajili ya kuezeka Zahanati Wilayani Mkuranga ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Benki hiyo kurudisha wanachopata kwa jamii ya wanaofanyanao biashara.

Amekabidhi Madiwati kwa Mgeni rasmi wa Maadhimisho ya sherehe ya siku ya Wanawake duniani kimkoa katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kisemvule Mkuranga Mkoani Pwani Mbunge Viti Maalumu mkoa wa Pwani Mheshimiwa Subira Mgalu Meneja wa Banki ya NMB Kanda Dar es Salaam na Pwani Seka Urio amesema msaada huo ni kwaajili ya Zahanati na Shule za Wilaya ya Mkuranga.

Amefafanua ugawaji wa msaada huo kwa Wilaya ya Mkuranga Urio amesema katika madawati 100 waliyokabidhi madawati 50 yatapelekwa Shule ya Kisemvule, madawati 25 Shule ya Msingi Chatembo na madawati mengine 25 yatapelekwa Shule Msingi Jamhuri, shule ya Sekondari Kiparang'anda watapata vitanda 20 vya dabo deka, mabati 100 kwaajili ya kituo cha Afya cha Kibugumo.

Akizungumza kwa niaba Mkuu wa Mkoa wa Pwani Alhaji Abubakari Kunenge, Mh. Subira Mgalu amewataka Wanawake Mkoani humo kusimamia maamuzi waliyojiwekea ya kumchagua Rais Mwanamke ambaye ni Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Subira amewaeleza wanawake waliofika kwenye sherehe hizo kuhakikisha ifikapo wakati wa uchaguzi mkuu wa 2025 wanamchagua Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na wenye sifa kujitokeza kugombea nafasi za ubunge na udiwani.

Amesema Rais Dkt. Samia anatosha anaweza na amefanya makubwa katika kuwezesha wananchi kiuchumi, msaada wa kisheria ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maendeleo katika sekta mbalimbali hapa nchini.

Amesema Rais Dkt .Samia katika Afrika Mashariki anaongoza kwa kutekeleza miradi ya kimkakati nchini ikiwemo miradi ya SGR, mradi wa kufua umeme la bwawa la Mwalimu Nyerere, miradi ya madaraja makubwa makubwa nchini na miradi mingi mikubwa ya maendeleo inaendelea vizuri kutekelezwa kilichobaki ni kuendelea kumshukuru na kumhakikishia kura za kishindo katika uchaguzi Mkuu ujao.

Mhe.Subira amesema Maadhimisho ya sherehe ya siku ya Wanawake duniani ni mwaka huu ni ya 114 tangu ilipoanza kusheherekewa mwaka 1911, ni sherehe ya 50 tangu ilipoanza kutambuliwa na Umoja wa mataifa, sherehe ya baada ya a miaka 30 ya mkutano wa Beijing ulikuwa chini ya Katibu Mkuu Mama yetu Getrude Mongela na sherehe ya kwanza hapa Nchini tukiwa na Mgeni rasmi Rais Mwanamke Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi huyo Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nasir Ally alimkabidhi Mhe.Mbunge Viti Maalum Subira Mgalu Tunzo ya madini ya Tanzanite kwaniaba ya Wananchi wa wilaya ya Mkuranga kwaajili ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mengi na makubwa aliyotekeleza katika kuwahudumia Wananchi Wilaya hiyo na kumuhakikishia wapo pamoja nae.

Sherehe hizo zimepambwa na maandamano ya Wanawake kutoka Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi ikiwa ni pamoja na TAKUKURU, PSSSF, NMB, CRDB, JKT RUVU, Mtandao wa Askari wa Jeshi la Polisi Pwani Shirika la Elimu Kibaha, Nyumbu, Wajasiriamali wote ndani ya Mkoa wa Pwani ambao walipata fursa ya kunesha bidhaa zao na Wajasiriamali Wanawake waliowezeshwa kwa mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmshauri za Mkoa huo.

No comments: