Maonesho ya Biashara za Wanawake na Vijana Tanzania Yaendelea, Kigahe Ahimiza Wajasiriamali Kutumia Fursa za Serikali

 

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe katikati akikata utepe kuashiria uzinduzi wa maonesho ya Biashara ya wanawake na Vijana yanayofanyika katika eneo la kuegesha magari Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Machi 03, 2024.

Na Avila Kakingo., Michuzi TV
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amekipongeza Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kwa juhudi zao za kuchochea uchumi wa nchi kupitia uwezeshaji wa wanawake na vijana wajasiriamali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 03, 2025 katika ufunguzi wa Maonesho ya Biashara za Wanawake na Vijana Tanzania, yaliyoandaliwa na TWCC, Kigahe aliwahakikishia wajasiriamali kuwa serikali iko bega kwa bega nao ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao na kuwa chachu ya maendeleo kama sehemu ya sekta binafsi.

Hii ni fursa kwa wajasiriamali wadogo na wale wanaotaka kuanzisha biashara zao kuonyesha ubunifu wao, bidhaa, na huduma wanazozalisha.

Azma ya maonesho hayo ni kusaidia kukuza biashara ndogo na za kati, kupanua fursa za ajira, na kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika uchumi wa taifa. Na ni hatua muhimu ya kuunga mkono jitihada za serikali za kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia ujasiriamali.

"Kote duniani tunatambua kuwa wajasiriamali wanazalisha bidhaa mbalimbali, zikiwemo bidhaa za mwisho zinazofika kwa walaji na bidhaa za kati zinazotumika viwandani. Ni muhimu kutumia fursa zilizopo ili kukuza sekta hii," alisema Kigahe.

Aidha, amewataka wajasiriamali kutumia fursa zinazotolewa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa serikali imejipanga kuboresha mazingira ya biashara na ujasiriamali nchini. Pia alizihimiza taasisi zinazohusiana na biashara kuendelea kusaidia wafanyabiashara kufanikisha malengo yao ya uzalishaji na masoko.

Kwa upande wake, Rais wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema kuwa maonesho hayo, yanayofanyika kwa mwaka wa tano mfululizo, yanatoa fursa kwa wanawake na vijana kubadilishana uzoefu, kujifunza, na kutafuta masoko mapya.

"Tunayo furaha kuona kuwa maonesho haya yamekutanisha wajasiriamali 300 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar. Hii ni fursa kubwa kwao kujifunza na kukuza biashara zao," alisema Hamza.

Naye Mkurugenzi wa TWCC, Mercy Silla, ametoa shukrani kwa serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara. Aidha, alibainisha kuwa chama hicho kimefungua dirisha maalum kwa vijana wa kiume wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ili kuwashirikisha katika ujenzi wa uchumi wa taifa.

Maonesho haya yanafanyika kila mwaka katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani na yanalenga kuwawezesha wanawake na vijana kujikita zaidi katika sekta ya biashara na ujasiriamali.
Naibu  Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 03, 2025 katika ufunguzi wa Maonesho ya Biashara za Wanawake na Vijana Tanzania, yaliyoandaliwa na TWCC.
Mkurugenzi wa TWCC, Mercy Silla akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 03, 2025 katika ufunguzi wa Maonesho ya Biashara za Wanawake na Vijana Tanzania, yaliyoandaliwa na TWCC.





Naibu  Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, akitembelea mabanda jijini Dar es Salaam leo Machi 03, 2025 wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Biashara za Wanawake na Vijana Tanzania, yaliyoandaliwa na TWCC.

No comments: