AU YAPONGEZA MCHANGO WA TANZANIA KATIKA KULETA AMANI NA USALAMA BARANI AFRIKA
Mwakilishi wa Kudumu wa Ufalme wa Morocco katika Umoja wa Afrika na Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama kwa mwezi Machi 2025 Mhe. Balozi Mohamed Arrouchi kwenye ufunguziwa mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama Umoja wa Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) yanayoendelea jijini Arusha Machi 25, 2025.
• Naibu Waziri Chumi ataja masuala sita muhimu kufika Afrika yenye amani na usalama wa kudumu
Umoja wa Afrika (AU) umeipongeza Tanzania kwa mchango wake wa kipekee wa kuleta amani na usalama wa kudumu katika maeneo mbalimbali barani Afrika.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 25, 2025 kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama Umoja wa Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) uliofanyika jijini Arusha.
Akitoa pongezi hizo Kamishina wa Masuala ya Siasa, Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika Mhe. Balozi Bankole Adeoye kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja huo Mhe. Azali Assoumani, ameeleza kuwa siku zote Tanzania imekuwa mstari wa mbele, ikijitoa kwa hali na mali katika kuongoza juhudi za kuleta amani na usalama barani Afrika.
Aliongeza kusema kuwa mchango huo unatokana na sera madhubuti na misingi imara iliyowekwa na Mwasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kuendelea kusimamiwa kwa ufanisi na uongozi mahiri wa sasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tuko hapa jijini Arusha leo sio kwa bahati mbaya, hii ni ishara ya kutambua na kupongeza rekodi ya kipekee ya Tanzania katika kuleta amani na usalama barani Afrika. Sote tunatambua tokea zama za kupigania uhuru, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mataifa mengi na ilitoa mchango wake wa hali na mali kuhakikisha mataifa mengine ya Afrika yakuwa huru. Juhudi hizo hazikuishia hapo, hadi leo Tanzania imeendelea kuwa kinara katika utatuzi wa migogoro sehemu mbalimbali ili kuhakikisha Waafrika wanafurahia matunda ya uhuru wao. Alisema Balozi Adeoye.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato David Chumi akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Waziri Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono bila kuyumba katika kutekeleza mipango ya Baraza la Amani na Usalama la AU kwenye kutimiza malengo ya agenda 2063 kuhusu Afrika yenye maendeleo endelevu.
Tanzania tumekuwa taifa ambalo mara kwa mara tanatetea “Amani na Umoja,” dhana ambayo inaonesha na kudhibitisha kujitoa kwetu katika kujenga, kulinda na kutetea misingi ya kutafuta amani na usalama wa kudumu barani Afrika bila kuchoka. Kiongozi wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassa ameendelea kuhimiza na kutekeleza hayo kwa vitendo. Alieleza Mhe. Chumi
Mbali na hayo Naibu Waziri Chumi amependekeza masuala sita muhimu ya kuzingatiwa na PSC ili kufikia Afrika yenye amani na utulivu wa kudumu. Masuala ni; umoja na mshikamano katika kuteleza majukumu, kuepuka kutoa kipaumbele kwa maslahi binafsi na utoaji wa michango ya fedha kwa wakati,
Masuala mengine muhimu ni; kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya Umoja wa Afrika na taasisi zingine za kikanda na kimataifa, utekelezaji mzuri wa makubaliano ya Amani yanayofikiwa na mwisho kuhakikisha ushirikishwaji wa makundi maalumu katika juhudi za kutafua amani na usalama wakiwemo vijana na wanawake.
Mafunzo hayo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama la AU yalianza Machi 23, 2025 na yanatarajiwa kufikia tamati Machi 27, 2025 yakilenga kuwajengea uwezo wajumbe hao kuhusu masuala mbalimbali muhimu ya kuwawezesha kutekeleza majukumu ya baraza hilo kwa ufanisi. Mafunzo najumuisha wajumbe wapya walioteuliwa hivi karibuni, pamoja na wengine kumi ambao wameendelea kutetea nafasi zao katika Baraza la Amani na Usalama la AU.
Aidha, Tanzania, ambayo imetumikia kama mwanachama wa Baraza la Amani na Usalama kwa kipindi cha miaka miwili, katika mafunzo hayo inawakilishwa na Ujumbe wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika ambao unaongozwa na Mhe. Balozi Innocent Shiyo
Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wajumbe hao, hasa wale walioteuliwa hivi karibuni kuhusu masuala mbalimbali muhimu ya kuwawezesha kutekeleza majukumu ya baraza hilo kwa ufanisi na tija zaidi ikiwemo kuelewa misingi na mamlaka ya PSC, kazi zake, mbinu za kufanya kazi na kushirikiana na Tume nzima ya AU na wadau wengine wa kikanda na kimataifa ikiwemo Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Mataifa.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU-PSC) liliundwa mwaka 2004 kupitia Itifaki ya kuanzishwa kwa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika. AU-PSC linawajibika kuzuia, kusimamia, na kutatua migogoro katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika. Programu hii ya mafunzo itajumuisha shughuli mbalimbali zitakazoongozwa na wanadiplomasia wakuu, wataalamu wa sera, na maafisa wa AU kwa lengo la kuwawezesha wajumbe kuelewa masuala muhimu ya PSC ikiwemo kuhusu muundo, majukumu na juhudi zinazofanyika ili kuleta amani na usalama endelevu barani Afrika.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Cosato David Chumi akifungua mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama Umoja wa Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) yanayoendelea jijini Arusha. Machi 25, 2025.
Balozi wa Tanzania nchini na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Hiyo akifuatilia mafunzo ya Wajumbe wa Baraza la Amani na Usalama Umoja wa Afrika – African Union Peace and Security Council (AU-PSC) yanayoendelea jijini Arusha Machi 25, 2025.
No comments: