TANESCO YAKAMILISHA MABORESHO YA UMEME MTAA WA PACHANNE B, RUVUMA
Na Belinda Joseph, Ruvuma
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limefanikisha kuboresha huduma ya umeme katika mtaa wa Pachanne B, kata ya Mjimwema, kwa kuongeza transfoma mpya ili kuondoa changamoto ya umeme hafifu katika eneo hilo.
Akizungumza katika mwendelezo wa ziara yake kwa wateja wa Shurika hilo Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Ruvuma Allan Njiro, amesema mabadiliko haya ni sehemu ya jitihada za shirika hilo kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa kutosha na wa kuaminika kwa matumizi yao ya kila siku.
Ameeleza kuwa Mabiresho hayo yameungwa mkono na Mama cha Urembo, ambaye alikubali kutoa eneo lake kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, na juhudi zake zimepongezwa na viongozi na wananchi wa eneo hilo.
Awali, mtaa wa Pachanne B ulikuwa na changamoto kubwa ya umeme hafifu kutokana na transfoma moja pekee ambayo ilihudumia viwanda na majumbani kwa pamoja, jambo lililosababisha usambazaji duni wa umeme na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Ili kuboresha hali hiyo, TANESCO imeongeza transfoma nyingine, hivyo sasa mtaa huo utafaidika na transfoma mbili, jambo linalowezesha mgawanyo bora wa umeme kwa matumizi ya viwanda na majumbani, na hivyo kuboresha huduma kwa wakazi wa mtaa huo.
Mwananchi wa mtaa wa Pachanne B, Saimon Gabriel Ndewele, ameshukuru TANESCO kwa kushughulikia tatizo la umeme na kumshukuru Mama cha Urembo kwa msaada wake.
Diwani wa kata ya Mjimwema, Silvester Mhagama, amesisitiza kuwa mradi huu utaongeza uzalishaji viwandani na kuboresha uchumi wa eneo hilo, na pia amepongeza serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuboresha huduma za umeme na miundombinu kwa wananchi.
No comments: