MPANGO KAZI WA HAKI ZA BINADAMU NA BIASHARA KUIMARISHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI TANZANIA

  

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mohamed Khamis Hamad akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mapitio ya mpango kazi wa haki za binadamu na biashara, kikao kazi hicho kimefanyika jijini Dar es Salaam leo Februari 21,2025.
Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Noel Komba akizungumza na waandishi wa habari namna mpango kazi wa haki za binadamu na biashara utavyonufaisha. Kikao kazi hizo kimefanyika jijini Dar es Salaam leo Februari 21, 2025.


SERIKALI inazidi kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha mazingira ya biashara nchini yanazingatia haki za binadamu, hali inayotarajiwa kuchochea uwekezaji na kuimarisha uwajibikaji wa makampuni kwa jamii. Katika hatua hiyo, Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Uandaaji wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na Biashara imekutana kupitia Rasimu ya awali ya mpango huo, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea utekelezaji wake rasmi.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mohamed Khamis Hamad akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Dar es Salaam, Februari 21, 2025 amesema mpango huo utatoa mwongozo kwa serikali na sekta binafsi katika kuimarisha biashara zinazozingatia haki za wafanyakazi, jamii, na uhifadhi wa mazingira.

“Tumefanya tathmini ya hali ya haki za binadamu katika sekta mbalimbali kama migodi, nishati, na viwanda ili kuhakikisha mpango huu unajibu changamoto zilizopo. Mpango kazi huu utakuwa nyenzo ya kuweka uwiano kati ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa watu,” alisema Hamad.

Kwa mujibu wa Mchumi Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Noel Komba, mpango huo utasaidia kuvutia wawekezaji kwani unaleta utulivu wa kibiashara kwa kupunguza migogoro inayohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu katika maeneo ya kazi.

“Huwezi kuwa na uwekezaji endelevu kama haki za wafanyakazi haziheshimiwi au kuna migogoro kati ya jamii na wawekezaji. Mpango huu utaimarisha mazingira ya uwekezaji kwa kuhakikisha kila mdau ananufaika bila kudhulumiwa,” alisema Komba.

Mpango huo, ambao unaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria Tanzania Bara na Zanzibar, unatarajiwa kuanza kutekelezwa kabla ya mwaka 2030. Unahusiana moja kwa moja na miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu na maazimio mengine ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Hatua hii inaashiria dhamira ya serikali ya kuhakikisha biashara zinakuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa kuheshimu haki za binadamu na kuhakikisha kuwa wafanyakazi na jamii zinakuwa sehemu ya mabadiliko chanya yanayoletwa na uwekezaji wa ndani na wa kimataifa.





Baadhi ya wajumbe kutoka idara na serikali wakijadiliana mpango kazi wa haki za binadamu na biashara.

No comments: