WAJASIRIAMALI SOKO LA TEGETA NYUKI WANUFAIKA NA ELIMU YA HIFADHI YA JAMII KUTOKA NSSF


Na MWANDISHI WETU,

 Lengo la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali ya wananchi linaendelea kwa kasi baada ya wajasiriamali katika soko ya Tegeta Nyuki, jijini Dar es Salaam, kuhamasika kujiwekea akiba baada ya kupata elimu kutoka NSSF ili waweze kunufaika na mafao.

NSSF kupitia kwa Meneja wa Sekta isiyo rasmi, Bi. Rehema Chuma imeweka kambi ya siku nne katika soko la Tegeta Nyuki na Kawe, lengo likiwa ni kutoa elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha wanachama wapya na kuhamasisha uchangiaji ambapo hamasa ya wajasiriamali kupata elimu na kujiunga imekuwa kubwa.

Akizungumza tarehe 8 Januari 2025, Bi. Rehema amesema katika muendelezo wa utoaji elimu kwa wajasiriamali NSSF imefika katika soko la Tegeta Nyuki kwa ajili ya kufikisha elimu kuhusu umuhimu wa wananchi kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye.

Amesema kuna namna mbili za mwanachama kujiunga moja wapo ni kujaza fomu na mwenye namba ya NIDA anaelimishwa kujisajili kwa kutumia mifumo, na kuwa mwanachama anaweza kuwasilisha michango kupitia simu ya kiganjani huko huko aliko ambapo kima cha chini cha kuchangia ni shilingi 30,000 ambapo atanufaika na fao la matibabu.

Baadhi ya wajasiriamali akiwemo Pastory Anthony ambaye ni mwanachama wa NSSF ananufaika na mafao yanayotolewa na Mfuko ikiwemo ya matibabu pamoja na familia yake.

Amesema kuna faida nyingi ambazo anazipata kwa kuwa mwanachama wa NSSF hivyo amewaomba wajasiriamali wengine kujiwekea akiba NSSF kwani ni mkombozi kwa kila mwanachama.

Naye, Bw. Marc Donald Maganga, Afisa Mkuu wa Sekta isiyo rasmi, amesema NSSF imeweka utaratibu nzuri wa wajasiriamali kujiunga na kuchangia ambapo mwanachama baada ya kujiandikisha anapewa namba ya kumbukumbu ya malipo na anapaswa kuchangia kuanzia shilingi 30,000 au 52,200 au zaidi kwa mwezi na anaweza kuchangia kidogo kidogo kwa siku, wiki, mwezi, muhula au msimu ili aweze kunufaika na mafao yote yanayotolewa ikiwemo ya uzee, urithi, uzazi, matibabu na msaada wa mazishi.
















No comments: