SITA WATUHUMIWA NA MASHTAKA 68 PAMOJA NA KUFANYA UDANGANYIFU WA MASHINE ZA EFD
VIJANA sita wanatuhumiwa na mashtaka 68 ya uhujumu uchumi yakiwemo ya kufanya udanganyifu kwenye mashine za kieletroniki EFD na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh bilioni 2.1 wanaendelea kusota rumande, upelelezi wa kesi yao bado haujakamilika.
Vijana hao ni mfanyabiashara Stanslaus Mushi (27) Mkazi wa Malamba mawili, Nemence Mushi (29), Rose Nanga (33), Mhasibu wa Soko Mkazi wa Kimara B, Hussein Mlezi (37) Fundi wa Kompyuta Mkazi wa Mbagala Kuu, Edwin Mark (22) Mkazi wa Yombo Vituka na Salim Salehe (45) Mchoraji.
Mashtaka wanayoshtakiwa nayo ni kutumia mashine za EFD kwa namna ambayo inapotosha mfumo na kamishna (64) kuisababisha TRA hasara (1) na kupata usajili wa namba ya utambulisho ya Mlipakodi (TIN) na usajili wa Ongezeko la Thamani (VAT) kwa njia ya uongo.
Wakili wa Serikali Rhoda Maingu akisaidiana na Wakili Auni Chilamula amedai leo Januari 20, 2025 mbele ya Hakimu Mkazi Amos Rweikiza wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam kuwa kesi hiyo iliitwa kwa kutajwa, upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Baada ya kudai hayo, Wakili wa mshtakiwa 1 na 2 Estei Madulu amedai kuwa suala la kutokukamilika kwa upelelezi limeshapitwa na wakati, kuna kitu kinaitwa haki jinai mshtakiwa akiletwa mahakamani upelelezi unakuwa umeshakamilika kesi inaendelea kusikilizwa.
"Sasa hapa tukubaliane mambo mawili aidha kesi iendelee au mpeleke kesi kwenye mahakama yenye mamalaka ya kusikiliza kuliko kusema tu upelelezi bado,"amedai Wakili Madulu
Hakimu Rweikiza aliwauliza mawakili wa serikali kama wasikia kilichozungumzwa na pia akasema Hakimu Mkazi Mkuu Radhamani Rugemalira anayesikiliza kesi hiyo amaepata udhuru ya kikazi yupo nje ya ofisini.
"Mshtakiwa mtarudishwa rumande hadi Februari 5, mwaka huu kesi yenu itakapotajwa,"amesema Hakimu Rweikiza
Mbali na Madulu mawakili wengine wanaowatetea washtakiwa ni Khalid Mzee na Jacob Minja.
Washtakiwa hao katika kosa la kwanza hadi 64 wanatuhumiwa kutenda kati ya Novemba Mosi na Novemba 30, 2024 wanatuhumiwa kufanya udanganyifu katika mashine ya EFD kwa lengo la kuupotosha mfumo na kamishna, mashine hiyo mali ya Hadija Songea ikionesha kufanya mauzo na kutoa lisiti mbalimbali.
Ilidaiwa kuwa katika shtaka la 65 na 66 linamkabili Mushi, Nanga na Salehe, wanatuhumiwa kupata usajili wa namba ya TIN yenye jina la Hadija Songea kwa njia ya uongo, wanadaiwa kufanya kosa hilo kati ya Juni Mosi na Juni 30, 2024.
Katika shtaka la 67 linawakabili mshtakiwa Mushi na Nanga wanatuhumiwa kufanya udanganyifu kwa kusajili mashine ya EFD kwa jina la Hadija Songea kosa hilo wandaiwa kutenda kati ya Juni Mosi na Juni 30, 2024.
Ilidaiwa kwamba katika shtaka la 68, washtakiwa wanadaiwa kati ya Novemba Mosi na Novemba 30, 2024 ndani ya jijini Dar es Salaam waliisababishia TRA hasara ya Sh. 2,160,310,567.51 kutokana na makosa ambayo wameyatenda ya matumizi ya uongo ya mashine ya EFD.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yao, hakimu aliwaeleza kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikilza kesi hiyo hivyo hawatakiwi kujibu chochote kuhusu mashtaka hayo.
No comments: