BONANZA LA WAFANYAKAZI TRA NA WAFANYABIASHARA KARIAKOO LAFANA

Timu ya Wafanyabiashara Kariakoo, wakishangilia baada ya kuibuka mabingwa wa bonanza la michezo la Siku ya Mlipakodi katika viwanja vya Michezo Jakaya Kikwete, jijini Dar es Salaam.

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mcha Hassan Mcha, akikabidhi kwa Nahodha wa timu ya Wafanyabiashara Kariakoo, Shafii Salimu, kombe baada ya kuifunga timu ya TRA, katika  michuano ya bonanza la Siku ya mlipakodi, viwanja vya Michezo Jakaya Kikwete, Dar es Salaam, jana. Wa tatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.


Wafanyabiashara wa Kariakoo na watumishi wa TRA, wakichuana katika mchezo wa kukimbia na magunia katika viwanja vya Michezo Jakaya Kikwete, jijini Dar es Salaam.



Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mcha Hassan Mcha, akikagua timu ya Wafanyabiashara Kariakoo na TRA, katika bonanza la michezo la kuazimisha wiki ya mlipakodi, viwanja vya Michezo Jakaya Kikwete, Dar es Salaam, jana. Mwenye miwani ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo.Timu hizo zilitoka suluhu.


WAFANYABIASHARA na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wapatao 500 wamejitokeza leo Januari 19, 2025 katika Bonanza la aina yake lililoandaliwa na Mamlaka hiyo ikiwa ni namna ya kudumisha ushirikiano, kuongeza hamasa na kutoa elimu kwa wadau wengine kulipa kodi kwa hiari.

Bonanza hilo lililofanyikia katika viwanja ya JK Youth Park, Kidongo Chekundu, lilitanguliwa na mbio za kilomita tano zilizoongozwa na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha aliyekuwa mgeni rasmi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo pamoja na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Severin Mushi.

Katika bonanza hilo, washiriki wamecheza michezo mbalimbali ikiwemo, mchezo wa Karata, Bao, kuvuta kamba, kukimbia na magunia, na mchezo wa mpira wa miguu.

Michezo mingine ilikuwa, drafiti, kukimbia na goroli kwa timu za wafanyabiashara wa Kariakoo, wafanyakazi wa TRA na wadau wengine.

Meneja Msaidizi wa TRA wa Mkoa wa Kikodi Kariakoo, ambao ndiyo waandaaji wa Bonanza, Edson Isanya amesema lengo la kufanya tukio hilo ni kudumisha uhusiano kati ya TRA na wafanyabiashara.

Akizungumzia Bonanza hilo, Mcha amesema wataendeleza ushirikiano kati yao na wafanyabiashara ilikuongeza mabilionea wanaolipa kodi kila mwaka.

"Mkoa wa kikodi Kariakoo ni mkoa wa kimkakati ambao katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/2025 imekusanya shilingi bilioni 71 .7 kwa kipindi cha miezi sita ya kwanza sawa na ufanisi wa asilimia 104 lengo hili limefanikiwa ikiwa ni kutokana na kusogeza huduma muhimu kwa Wafanyabiashara 30000 wanaotegemea soko hilo.

"Kama tunavyojua soko hili linategemewa na watu kutoka Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika pamoja na Visiwa vya Comoro,"amesema Mcha

Amesema, Kariakoo itaendelea kuwa kiungo muhimu ukilinganisha ni mikoa mingine ya Kodi, hivyo kwa kuzingatia hilo TRA itaendelea kushirikisha wadau mbalimbali kwenye matukio ya pamoja ilikukuza, kuimarisha uhusiano uliopo kati ya sekta binafsi na Mamlaka ili mabilionea waendelee kuongezeka kila Mwaka.

Mcha pia amewashukuru wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari kukuza pato la Taifa na kuhaidi kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kufanya kazi kwa uweledi na ubunifu na kupitia mikakati yote waliyoiweka ikiwemo kuongeza mabilionea kila mwaka na mwisho mabilionea hao waende idara ya kati na kubwa ya ulipaji kodi.

Alisema wataendelea kuongeza idadi ya wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi, kuongeza huduma mashine za EFD pamoja na wafanyabiashara wadogo(Machinga).

"Tunamikakati mbalimbali ilikusaidia walipa kodi, kusaidia wamachinga na wengine kutoka ndani na nje ya nchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari bila changamoto,"amesema

Kwa upande wake, Mkuu Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema, serikali itaendele kushirikiana kwa ukubwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanashirikiana na ofisi ya Mkuu wa mkoa wa dar es salaam kuhamasisha ulipaji kodi kwa wafanyabiashara ukizingatia kuwa mkoa huo ndio unaoongoza kwa walipa kodi.

Amesema pia wataimarisha mazingira bora kwa Wafanyabiashara ili waweze kulipa kodi stahiki.

Amesema katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia Wilaya ya Ilala imepokea Sh bilioni 305 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu,afya na barabara.

"Katika fedha hizo tumejenga madarasa,tumelipia watoto elimu ya msingi na sekondari,vituo vya afya na mengine mengi,TARURA walikuwa wanapata kiwango kidogo cha fedha lakini kwa kipindi hiki fedha zimeongezeka hadi kufikia bilioni 20 na hizi zote ni kutokana na juhudi za mama Samia ni wazi lazima tumpongeze na niongezeko kubwa lililotokana na ukusanyaji mzuri wa Kodi unaofanywa na TRA,"amesema Mpogolo.

Amesema kwa mwaka 2025 halmashauri ya Jiji wanatarajia kuvuka lengo kutoka Sh bilioni 111 hadi bilioni 120 sababu ya mashirikiano mazuri na makubwa kutoka kwenye kila taasisi zote za serikali.

Alisema ni wazi Rais Samia amekuwa kinara Duniani, Afrika na Januari 26, 27 na 28 atakuwa na ugeni mkubwa wa maraisi kutoka barani Afrika, viongozi kutoka Mataifa mbalimbali hivyo wafanyabiashara jiandaeni vizuri kumheshimisha Rais.

Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya na Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severin Mushi amesema wamevunja rekodi nyingi mwaka uliopita na sasa wako tayari kulipa kodi bila kamata kamata kwani majadiliano na mikutano iliyofanyika na Mamlaka imeleta matokeo mazuri kwa walipa kodi wote.

No comments: