Watu Wenye ulemavu wametakiwa kutumia fursa ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura

Mbunge viti maalum kundi la watu wenye ulemavu anaewakilisha Tanzania nzima Stella Ikupa Alex akizungumza leo Desemba 17, 2024 mara baada ya kukabidhi kompyuta kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)katika Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui.


Na Nihifadhi Abdulla Zanzibar.
WATU wenye ulemavu wametakiwa kutumia fursa yao ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili ili waweze kupata haki yao ya msingi ya kupiga kura.

Mbunge viti maalum kundi la watu wenye ulemavu anaewakilisha Tanzania nzima Stella Ikupa Alex alieleza hayo wakati akikabidhi kompyuta kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)katika Ofisi kuu ya CCM Kisiwandui.

Alisema hatua hiyo pia itawawezesha kupigiwa kura watakapoweza kujitokeza kugombea nafasi ambazo zipo ndani ya chama nan je ya chama.

Aidha alibainisha kuwa Chama cha Mapinduzi kinajali kundi la watu wenye ulemavu na kinatoa nafasi kwa watu hao ili kuona nao wanatoa mchango wao katika Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na hata katika Baraza la Wawakilishi.

“Wananchi wameanza kutufahamu watu wenye ulemavu, wanajua uwezo wetu na kufahamu kuwa mtu mwenye ulemavu akipewa nafasi anaweza akaitendea haki na kuifanya vizuri tujiamini kwamba tunaweza na kujitokeza kugombea tupigiwe kura na tuweze kupiga kura,” alisema.

Akizungumzia vifaa alivyotoa alisema lengo lake ni kuongeza nguvu kwenye jumuiya hiyo.

Aidha alisema chama cha Mapinduzi kinaelekea katika uchaguzi mkuu wa 2025 hivyo anaamini vifaa hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi taarifa muhimu na kutunza usiri wa ofisi zao.

Alisema tayari kompyuta hizo ameshakabidhi kwa upande wa UWT Tanzania bara na ameona kwa heshima ya Muungano wao basi na upande wa Zanzibar waweze kupata kwa ajili ya kusaidia katika majukumu yao ya kila siku ya jumuiya.

Aliwapongeza viongozi wa umoja huo kwa Tanzania bara na Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya kuisimamia jumuiya hiyo na kupata mafanikio makubwa.

Naye Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake anaefanyia kazi zake Zanzibar, Tunu Juma Kondo, alimpongeza mbunge huyo kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vimekuja wakati muafaka na vinahitajika hasa kipindi kinachokuja cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2025.

Alisema mbunge huyo amefanya uamuzi sahihi wa kutoa vifaa hivyo vya kompyuta na amekuwa akisaidia sana watu wenye ulemavu wa Zanzibar na kufata nyayo za Mwenyekiti wa CCM na Makamu wake kwani mara nyingi wamekuwa wakitoa vifaa vya kufanyia kazi ili kuona jumuiya zote za CCM zinafanya kazi vizuri.

Naibu Tunu alisema ni imani yake mbunge huyo ataendelea kusaidia kundi hilo la watu wenye ulemavu kwa upande wa Zanzibar.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka makatibu wa umoja huo kwa mikoa sita ya Unguja na Pemba ambao watakabidhiwa vifaa hivyo kuhaskikisha wanazihifadhi vizuri, kuzifanyia kazi na kuzitunza ili ziweze kusaidia katika majukumu yao ya kila siku.

Naye Katibu wa UWT Mkoa wa Mjini Mary Miwa na Katibu wa UWT Magharibi Salama Fadhil Juma walimpongeza Mbunge huyo kwa kuwapatia vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kwa kiasi kukubwa katika kazi zao za kila siku.

Walisema mbunge huyo amefanya jambo jema kuwapatia vifaa hivyo kwani walikuwa wakipata changamoto kuweka takwimu za wanachama zikiwa zimeandikwa kwa mkono hivyo hivi sasa kazi zao wataziweka kwa umahiri mkubwa.

Waliahidi kuwa watahakikisha wanavitunza vifaa hivyo na kuzifanyia kazi kama ilivyokusudiwa ili viweze kuwasaidia hasa katika kipindi cha uchaguzi katika kuweka takwimu za wanachama.

Komputa hizo saba zitagaiwa katika mikoa sita Unguja na Pemba na Uwt Taifa itapatiwa kompyuta moja ambazo zimegharimu zaidi ya shilingi 11,000,000.

No comments: