DAIMA CCM ITAZINGATIA WANANCHI: BALOZI NCHIMBI

-Asema huo ni msingi wa Watanzania kuendelea kuiamini CCM

-Atoa maelekezo mafunzo viongozi Serikali za Mitaa nchi nzima

-Apongeza Nzega Mjini utekekezaji wa Ilani ya Uchaguzi

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema siku zote CCM itazingatia maslahi na matakwa ya watu katika kuwatumikia Watanzania.

Balozi Nchimbi amesisitiza kuwa lazima CCM iendelee kujiakisi kuwa ni chama kinachoheshimu watu, kuwa tayari kuwatumikia, kwa kuzingatia maslahi, mahitaji na matakwa mapana ya wananchi.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la Nzega Mjini uliofanyika leo Ijumaa, tarehe 20 Desemba 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM Wilaya ya Nzega, Nzega Mjini, Balozi Nchimbi alieleza kuwa msingi wa mafanikio ya CCM ni kujikita katika mahitaji ya wananchi.

Akiwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo, alitoa maelekezo kwa uongozi wa CCM mkoani Pwani kuhakikisha wanarudia kura za maoni katika Kitongoji cha Mkoga, wilayani Mkuranga, baada ya mgombea wa CCM aliyeshindwa kukubalika kwa wananchi kuteuliwa tena.

“Mkoa wa Pwani, katika kitongoji kinachoitwa Mkoga, Wilaya ya Mkuranga, mgombea wa CCM ameshindwa katika uchaguzi wa wananchi. Halafu leo asubuhi nimetaarifiwa wamemteua tena kwenda kugombea. Hii ni dharau kwa wananchi na inakiuka misingi yetu ya kuheshimu matakwa yao.

“Natoa maelekezo, uchaguzi urudiwe, na mgombea aliyekataliwa na wananchi asishiriki katika kura za maoni za CCM,” alisema Balozi Nchimbi huku akisisitiza umuhimu wa CCM kujiakisi kama chama kinachowaheshimu na kuwatumikia watu.

Aidha, Balozi Nchimbi aliagiza viongozi wa Chama na Serikali kuhakikisha viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji waliochaguliwa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwezi uliopita, wanapewa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.

Katika mkutano huo, Mbunge wa Nzega Mjini, Mhe. Hussein Mohamed Bashe, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi jimboni. Balozi Nchimbi aliwapongeza mbunge ,viongozi wa Chama na Serikali wa Wilaya ya Nzega kwa jitihada zao za mshikamano, umoja, na kuimarisha imani ya wananchi kwa CCM.

Mapema kabla, Balozi Nchimbi alifanya uzinduzi wa ukumbi mkubwa wa mikutano unaomilikiwa na CCM Wilaya ya Nzega, wenye uwezo wa kutumiwa na watu takriban 1,500 - 1,900 wakiwa wamekaa.

Aidha, Balozi Nchimbi aligawa nyenzo za kazi, aina ya pikipiki zipatazo 229, zilizotolewa na Mhe. Bashe kwa viongozi wa Chama na jumuiya zake katika ngazi ya kata na matawi, pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Mitaa, katika Jimbo la Nzega mjini.









No comments: