WANAFUNZI WA KIKE SEKONDARI WAJENGEWA UWEZO AFYA YA KIDIJITALI
Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Ufundi, Idara ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Mwajuma Lingwanda akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la nne la ya Afya ya Kidigitali na Ubunifu katika Chuo Kikuu Kishiriki Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo,. Kongamano hilo limefanyika leo Novemba 11,2024 katika chuo cha Muhas Jijinj Dar es Salaam
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Profesa Emmanuel Balandya akizungumza na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa kongamano la nne la ya Afya ya Kidigitali na Ubunifu katika Chuo Kikuu Kishiriki Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo,. Kongamano hilo limefanyika leo Novemba 11,2024 katika chuo cha Muhas Jijinj Dar es Salaam.
Debora Enock Mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Mbezi Inn akizungumza wakati wa kongamano hilo.
Kalyne Mseki, mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule ya sekondari Jangwani, akizingumza wakati wa kongamano hilo.
Na Mwandishi Wetu Michuzi Tv
WAKATI matumizi ya Teknlojia yakipamba moto nchini serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu kishiriki cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) imeanza mkakati wa kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike kutoka shule za sekondari katika utafiti , ubunifu na maendeleo katika teknolojia ya Afya kidigitali.
Wanawake husani wanafunzi wa kike wakijengewa uwezo basi wanaweza kuwa vinara wa teknolojia.
Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Ufundi, Idara ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Dkt. Mwajuma Lingwanda
amesema hayo leo Novemba 11,2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la nne la ya Afya ya Kidigitali na Ubunifu katika Chuo Kikuu Kishiriki Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, Dkt. Lingwanda amesema kuwa Afya ya kidijitali inabadilisha haraka mifumo utoaji wa huduma za afya.
“Kama ilivyo kwa nchi nyingine, Tanzania imeandaa na inatekeleza mkakati wa afya ya kidijitali wa 2019-2024, ambao pamoja na mambo mengine, unahimiza elimu, utafiti, ubunifu na maendeleo katika teknolojia za afya kidijitali ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa afya bora ya jamii” .
Amesema kuwa wizara hiyo inaunga mkono mpango huo kwa kwa kuwa umelenga kumnyanyua mwanamke ili akabiliane na matakwa ya kidunia.
“Wizara yangu inauunga mkono maono haya. Tutaendelea kuhamasisha elimu ya STEM kwa wasichana, kupanua upatikanaji wa rasilimali za kidijitali, na kujenga majukwaa yanayohamasisha uvumbuzi na uongozi miongoni mwa wanawake. Tumejipanga kuunda mazingira ambako mabadiliko ya kidijitali yanakuwa kichocheo cha usawa wa kijinsia na maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania.
“Wanawake na wasichana ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu wetu, hivyo lazima wahusishwe katika mabadiliko ya kidijitali endapo tunatarajia mapinduzi ya kidijitali. Lakini hili ni suala pana, si suala la teknolojia pekee bali linagusa moyo wa usawa, uwezeshaji, na maendeleo ya binadamu,’’amesema Dkt Lingwanda
Shule za Sekondari ya wasichana ya Jangwani, Mbezi Inn na Amosi makala zimeshiriki Kongamano hilo lenye kauli mbiu ‘Kuweka Daraja: Kuunganisha Wanawake na Wasichana katika Mustakabali wa Kidijitali’
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Emmanuel Balandya amesema ipo haja ya kuhakikisha mifumo ya hospitali zote nchini inakuwa kidijitali na kusomana ili kurahisisha utoaji wa huduma ili hata mgonjwa akipata dharura na kuhamishwa kutoka hospitali moja kwenda nyingine taarifa zake zipatikane kwa urahisi na siyo kuanza upya.
“Katika sekta ya afya bado hatufanyi vizuri katika suala la utunzaji na utoaji wa taarifa aidha za wagonjwa na kumbukumbu nyingine, tunahitaji kushughulikia suala hili, kusaidia utunzaji wa taarifa kidigitali badala ya kuhifadhiwa kwenye vitabu,”aliongeza Prof. Balandya.
"Kumbukumbu ni kitu cha msingi sana katika huduma za afya, ingawa tumeingia kutumia zama za kidigitali lakini bado haijafanikiwa kwa kiasi kikubwa, huduma nyingi za kiafya bado hazijawa kidijitli, kila hospitali ina mfumo wake ama wa karatasi au digitali lakini haisomani. Ameongeza
Prof. Balandya amesema, wataendelea kuzalisha wataalam kwa ajili ya kusaidia kuingiza mifumo yote inayotoa huduma za kijamii kusomana kigitali kwa kuzingatia miongozo ya Serikali.
Amesema katika utafiti waliofanya waliona ushiriki mdogo wa wanawake na mabinti katika matumizi ya teknolojia hivyo wameona ni vema wakaanza mapema kuwatengeneza wataalam kuanzia chini hususani watoto wa kike ambao ushiriki wao katika masomo ya sayansi ni mdogo.
"Kupitia mkakati wa kuwajengea uwezo watu mbalimbali, mwaka huu tumeweka msisitizo kwa wasichana kutoka Shule mbali mbali za sekondari ambao tutawapatiwa mafunzo ya jinsi ya kutumia Tehama kwenye kutafuta suluhisho za changamoto katika sekta ya Afya na kuongeza idadi na kulisaidia taifa kuwa na wataalam wataosaidia mifumo hiyo,” amesema Prof. Balandya.
Prof. Balandya amesema kongamano hilo lilianza mwaka 2021 na kwa sasa ni mara ya nne kufanyika ambapo mwaka huu litanyika pia na Zanzibar na kusaidia kuboresha mifumo ya digitali kusomana katika kila sekta.
Naye, Kalyne Mseki, mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka shule ya sekondari Jangwani, ameishukuru MUHAS kwa kuwapelekea elimu hiyo na kuongeza kuwa katika kuhakikisha kuna idadi kubwa ya wasichana katika matumizi ya digitali ni muhimu Serikali kwa kushirikiana na wadau wakawekeza kwenye ununuzi wa vifaa shuleni.
Amesema hatua hiyo itawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kujua namna masuala ya teknolojia yanafanya kazi na kuwahamasisha kutumia maarifa hayo hata wanapohitimu shule.
“ Tunafurahi kuwa sehemu ya kongamano hili, ni kweli kuwa idadi yetu wasichana katika matumizi ya teknolojia ni ndogo lakini mpango huu utatuhamasisha lakini ili kufikia malengo hayo lazima uwekezaji katika vifaa ufanyike kwa kuzingatia pia watu wenye ulemavu, shule ziwe na teknolojia kwa ajili ya kujifunza,” amesema Kalyne.
Debora Enock Mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Mbezi Inn, amesema mafunzo hayo ni muhimu kwao kwani yatawasidia kujua ni kwa namna gani wataitumia digitali kupata taarifa katika sekta ya afya.
No comments: