KWA MARA YA NNE TAMWA ZNZ YAZINDUA TUZO KWA WAANDISHI WA HABARI KUKUZA USAWA WA KIJINSIA

 



Na. Nihifadhi Abdulla, Zanzibar
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Jumuiya ya Wanasharia Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) imetangaza uzinduzi wa Tuzo ya uwiano wa kijinsia kwa Vyombo vya Habari "Media for Gender Equity Awards"

Akitoa Tara fa hiyo kwa vyombo vya habari huki Tunguu Mkurugenzi wa TAMWA Dkt. Mzuri Issa amesema tuzo hiyo yenye ujumbe "Kalamu Yangu, Mchango Wangu kwa Wanawake." itatambua vyombo vya habari na waandishi wa habari Zanzibar vinavyoandika na kuleta maudhui, changamoto, michango ya wanawake katika uongozi, na vinavyoshiriki kikamilifu katika kukuza usawa wa kijinsia kupitia kazi zao.

Aidha amesema Kupitia tuzo hiyo, TAMWA ZNZ inalenga kuhamasisha vyombo vya habari na waandishi wa habari kuunga mkono sauti za wanawake na kukuza uandishi wa habari wenye kuzingatia usawa wa kijinsia ili kuchangia mabadiliko ya kijamii kwa kuonesha nafasi za wanawake na uwezo wao katika uongozi ili kuleta maendeleo.

Amefafanua kuwa Mara hii tuzo hizo zinalenga kutambua vyombo vya habari vyenye mtiririko mzuri wa kusaidia kuongeza wanawake katika nafasi za uongozi. Hivyo vigezo vitakavyotumika ni kuwa na sera ya kijinsia, dawati la kijinsia, zana za tathmini na ufuatiliaji wa masuala ya usawa wa kijinsia, idadi ya habari zilizoaandikwa kuhusu wanawake na uongozi na nafasi ya wanawake waandishi wa habari katika chombo cha habari.

Maombi hayo yamefunguliwa leo na kazi zitaendelea kupokelewa hadi tarehe 5 Januari, 2025 ambapo Dkt Mzuri amesema Waandishi wa habari wanaweza kuwasilisha kazi zao ambazo zimezalishwa kuanzia Januari hadi Disemba, 2024 moja kwa moja Ofisi za TAMWA ZNZ zilizopo Tunguu na Mkanjuni Chakechake, Pemba

Tuzo hizo ambazo ni mara ya nne kufanyika zinafanywa kupitia mradi wa Kuwajengea Wanawake Uwezo katika Uongozi (SWIL) kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway.

No comments: