USHIRIKIANO WA TIC, TRA, TPSF KUHAMASISHA UWEKEZAJI NCHINI

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Binilith Mehenge akizungumza wakati wa mkutano maalum uliowakutanisha wawekezaji wa nje waliowekeza nchini, Mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 31, 2024.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Yusuph Mwenda akizungumza  wakati wa mkutano maalum uliowakutanisha wawekezaji wa nje waliowekeza nchini, Mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 31, 2024.
Mkurugenzi wa Ufanikishaji Uwekezaji, TIC, Revocutus Rashel akizungumza akizungumza wakati wa mkutano maalum uliowakutanisha wawekezaji wa nje waliowekeza nchini, Mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 31, 2024.

KITUO cha uwekezaji Tanzania-(TIC)kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA  pamoja na sekta binafsi (TPSF) kuboresha mazingira ya biashara, kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TIC, Binilith Mehenge wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 30, 2024. Mara baada ya awamu ya kwanza ya mkutano maalum uliowakutanisha wawekezaji wa nje waliowekeza nchini kumalizika. 

Amesema kuwa  ushirikiano huo  utachangia kwenye maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

Pia Mahenge amesisitiza umuhimu wa kuwa na mashirikiano ya pamoja katika usimamizi na kukuza uwekezaji nchini. 
  
"Mfumo huo wa mshikamano ni hatua muhimu ya kuwezesha maendeleo endelevu na kuongeza nafasi za ajira kwa Watanzania." Ameeleza Mahenge

Pia amezungumzia madhumuni ya  mkutano huo kuwa sehemu kubwa ni kuonyesha kwamba tupo tayari kufanya kazi na wawekezaji, kuondoa changamoto zote zilizopo katika mazingira ya uwekezaji.

"Tunaamini kwa pamoja sisi Taasisi ambazo zinasimamia kwamba  TIC, TRA na TPSF tunaonyesha mshikamano na tupo pamoja katika kusimamia suala la uwekezaji katika nchi yetu.” Amesema

Amesema mashirikiano hayo yanawapa taswira kwamba wawekezaji bado wanaimani na serikali ya Tanzania ndiyo maana wamekuja kusikiliza na kutoa maoni yao katika mkutano maalumu. 

Amesema kuwa suala la uwekezaji na biashara katika karne ya 21 ni jambo linaloshindaniwa kwa nguvu katika dunia nzima. Hivyo, wanaendelea kuwahamasisha wawekezaji wasije wakaishia tu kufungua miradi mipya, bali wahakikishe wanapanua na kuiendeleza miradi hiyo kwa manufaa ya muda mrefu.

“Tunawahamasisha wawekezaji wasiishie  kufungua mradi bali waweze hata kupanua mradi yao zaidi.” Amesema

Amesema muitikio wa wawekezaji kutoka nje kuja shiriki katika mkutano huo ni mkubwa kutokana na imani kubwa ya serikali ya awamu ya sita iliyo chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ilivyoweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa (TRA) Yusuf Mwenda aliwahakikishia wawekezaji hao wa nje kuwa wataendelea kujenga mahusiano mazuri nao, kwani TRA inashirikiana na TIC kuhakikisha kuwa wawekezaji wanakuja kuwekeza nchini, kuongeza idadi ya walipa kodi na pia kuhakikisha kuwa wawekezaji hao wanapata faida.

Pia amesema wataendelea kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kurahisisha shughuli za uwekezaji, kwa kuwa wawekezaji wa nje, kama walivyo wawekezaji wa ndani, wana mchango mkubwa katika uchumi kupitia kodi, ajira, na kuhamasisha shughuli za kiuchumi.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Rafael Mwenda  ameeleza  kuwa hapo awali kulikuwa na changamoto za kikodi ambazo wawekezaji walikuwa wakipitia. 


Licha ya hilo, kupitia majadiliano yanayoendelea, kuna mabadiliko makubwa yanayofanyika ambayo yanatarajiwa kuondoa changamoto hizo, hasa katika eneo la ukusanyaji wa kodi.

Pia ameshukuru serikali kwa kuanzisha Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Kodi, akisisitiza kuwa wao kama Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), wanajitahidi kuhakikisha kuwa maoni ya wafanyabiashara kuhusu masuala ya kodi yanazingatiwa na kushughulikiwa ipasavyo.

"Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa mfanyabiashara analipa kodi stahiki na ya haki, isiyo na dhuluma, ili aweze kukuza biashara yake na kuchangia katika maendeleo ya uchumi wa nchi." Amesema Maganga






Matukio mbalimbali katika mkutano maalum uliowakutanisha wawekezaji wa nje waliowekeza nchini.

No comments: