NECTA WATANGAZA MATOKEO YA DARASA LA SABA, WAVULANA WAONGOZA, 16 WAANDIKA MATUSI
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Said Mohamed akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 29,2024, wakati wa kutangaza matokeo ya mtihani wa Darasa la saba kwa mwaka 2024 mtihani uliofanyika Septemba.
BARAZA la Mitihani lTanzania (Necta) latangaza matokeo ya darasa la saba, ambapo mtihani ulifanyika Septemba 2024.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 29,2024, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Said Mohamed amesema kuwa jumla ya watahiniwa 1,230,774 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi wakiwemo Wasichana 666,597 sawa na asilimia 54.16% na Wavulana 564,177 sawa na 45.84. Kati ya watahiniwa waliosajiliwa, watahiniwa wenye mahitaji maalum walikuwa 4,583 sawa na asilimia 0.37 na Kati ya watahiniwa 1,230,774 waliosajiliwa, watahiniwa 1,204,899 sawa na asilimia 97.90 walifanya mtihani wakiwemo Wasichana 656,160 sawa na asilimia 98.43 na Wavulana 548,739 sawa na 97.26.
Aidha, Watahiniwa 25,875 sawa na asilimia 2.10 hawakufanya Mtihani, kati yao Wavulana ni 15,438 (2.74%) na Wasichana 10,437 sawa na asilimia 1.579.
Amesema jumla ya watahiniwa 974,229 sawa na asilimia 80.87 yawatahiniwa wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2024. Hivyo, ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.29. Kati ya watahiniwa 974,229 waliofaulu, Wavulana ni 449,057 sawa na asilimia 81.85 na Wasichana ni 525,172 sawa na asilimia 80.05.
Hivyo Ufaulu wa Wasichana umeshuka kwa asilimia 0.53 na ufaulu wa Wavulana umeongezeka kwa asilimia 1.26.
Ubora wa ufaulu kwa watahiniwa waliopata madaraja ya A na B umeimarika ambapo watahiniwa 431,689 sawa na asilimia 35.83 wamepata madaraja ya A na B ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.65 ikilinganishwa na mwaka 2023. Kati ya watahiniwa 431,689 waliopata ubora wa ufaulu katika madaraja ya A na B, Wasichana ni 216,568 sawa na asilimia 33.01 ukiwa na ongezeko la asilimia 9.09 na Wavulana ni 215,121 sawa na asilimia 39.21 wakiwa na ongezeko la asilimia 8.28 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Licha ya hayo Katibu Mtendaji akizungumzia matokeo yaliyozuiliwa amesema, Baraza la Mitihani la Tanzania limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 418 ambao waliugua au kupata matatizo mbalimbali na kushindwa kufanya Mtihani kwa idadi kubwa va masomo au masomo yote.
Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kurudia kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2025 kwa mujibu wa Kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani.
Kwa matokeo yaliyofutwa Baraza la Mitihani la Tanzania limefuta matokeo yote ya watahiniwa 45 ambao walibainika kufanya udanganyifu katika Mtihani kwa mujibu wa Sheria za Baraza la Mitihani na Watahiniwa 16 walioandika lugha va matusi katika skripti zao za majibu.
Akizungumzia idadi ya shule kimakundi Dkt. Mohamed amesema idadi ya Shule katika Makundi ya Umahiri Kati ya shule 18,932 zenye matokeo ya PSLE 2024, shule nyingi ambazo ni 12,838 sawa na asilimia 67.81 zimepata wastani wa Daraja la C ikilinganishwa na madaraja mengine ya ufaulu.
Shule zilizopata wastani wa Daraja la A-C ni 17,483 sawa na asilimia 92.35. Aidha, shule zilizopata wastani wa madaraja ya A na B zimeongezeka kwa asilimia 7.28 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Dkt. Mohamed akizungumzia kuhusiana na ufaulu wa watahiniwa kimasomo amesema Ufaulu wa somo la Kiswahili ni mzuri ambapo asilimia 86.58 ya watahiniwa wamefaulu.
Katika somo la English Language ufaulu umeendelea kuimarika kwani asilimia 43.48 ya watahiniwa wamefaulu ambapo ufaulu wa somo hilo umeongezeka kwa asilimia 9.13.
Ufaulu wa Wavulana na Wasichana katika somo la Kiswahil na English Language unawiana kwani Wasichana wamefaulu zaidi kuliko Wavulana kwa asilimia 0.36. katika Somo la Kiswahili na somo la English Language Wavulana wamefaulu zaidi kuliko Wasichana kwa asilimia 0.25.
Ubora wa ufaulu unaonesha kuwa, watahiniwa waliopata madaraja ya A na B katika somo la Kiswahili ni asilimia 53.46 ikilinganishwa na asilimia 69.41 katika mwaka 2023.
Katika somo la English Language watahiniwa waliopata madaraja hayo ni asilimia 15.25 ikilinganishwa na asilimia 11.40 katika mwaka 2023.
Kwa Masomo ya Sayansi Jamii ufaulu wa masomo ya Sayansi Jamii ni mzuri, ambapo asilimia 81.91 ya watahiniwa katika somo la Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi wamefaulu na katika somo la Uraia na Maadili watahiniwa waliofaulu ni asilimia 79.68. Katika somo la Maarifa ya Jamii na Stadi za kazi wavulana wamefaulu zaidi kuliko wasichana kwa asilimia 3.59.
Aidha, somo la Uraia na Maadili lina tofauti ndogo ya ufaulu kati ya Wavulana na Wasichana kwani Wavulana wamefaulu zaidi kuliko Wasichana kwa asilimia 0.14.
Ufaulu wa somo la Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi umeongezeka kwa asilimia 4.51 na katika somo umeshuka kwa asilimia 2.44 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Ubora wa ufaulu unaonesha kuwa, watahiniwa waliopata madaraja ya A na B katika somo la Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi ni asilimia 43.59 ikilinganishwa na asilimia 35.68 katika mwaka 2023. Katika somo la Uraia na Maadili watahiniwa waliopata madaraja hayo ni asilimia 46.97 ikilinganishwa na asilimia 42.53 katika mwaka 2023.
Kwa upande wa Masomo ya Sayansi na Hisabati, Ufaulu wa somo la Sayansi na Teknolojia ni mzuri ambapo asilimia 83.75 ya watahiniwa wamefaulu na katika somo la Hisabati ufaulu umeendelea kuimarika kwani asilimia 55.12 ya watahiniwa wamefaulu.
Aidha, katika somo la Hisabati Wavulana wamefaulu zaidi kuliko Wasichana kwa asilimia 6.03 na katika somo la Sayansi na Teknolojia Wavulana wamefaulu zaidi kuliko Wasichana kwa asilimia 3.61.
Ufaulu katika somo la Sayansi na Teknolojia umeongezeka kwa
asilimia 9.67 na katika somo la Hisabati umeongezelka kwa asilimia 6.29 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Ubora wa ufaulu unaonesha kuwa, watahiniwa waliopata madaraja ya A na B katika somo la Sayansi na Teknolojia ni asilimia 48.83 ikilinganishwa na asilimia 28.11 katika mwaka 2023.
Katika somo la Hisabati watahiniwa waliopata madaraja hayo ni asilimia 22.53 ikilinganishwa na asilimia 10.88 katika mwaka 2023.
No comments: