SUMA JKT WAUNGA MKONO KAMPENI YA SAMIA NIVISHE KIATU


Na Khadija Seif,Michuzi TV

TAASISI ya Mama ongea na mwanao ikiongozwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Steven Mengere amepokea jozi 500 ya viatu kutoka Shirika la uzalishaji mali la jeshi la kujenga taifa (SUMAJKT) ikiwa sehemu ya kuunga mkono Kampeni ya "Samia nivishe kiatu" kwa wanafunzi mashuleni hasa vijijini.

Akizungumza na Waandishi wa habari, Makao makuu ya Shirika la uzalishaji Mali la jeshi la Kujenga taifa (SUMAJKT)Jijini Dar es salaam Mkurugenzi Muendeshaji wa kiwanda cha viatu  na bidhaa za ngozi SUMAJKT Meja Mathias Peter John amesema wameona dhamira ya kushirikiana na taasisi ya 'Mama ongea na mwanao' kuunga mkono na kuonyesha uzalendo kuhakikisha wanafunzi mashuleni hasa vijijini wanapata viatu kutoka viwanda vya kinyumbani.

"Hatuwezi kusubiri wachina watuvalishie watoto wetu viatu hivyo tumeamua kwa dhati kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa na taasisi hiyo kupitia Mwenyekiti Steven Mengere kuvalisha watoto wa shule za vijijini viatu na tutahakikisha tunatengeneza jozi za kutosha katika Kiwanda cha uzalishaji wa viatu vya ngozi (SUMA JKT ) kuwapa thamani watoto wetu."

Hata hivyo Meja Mathias ameongeza kuwa amekabidhi jozi 500 za viatu vya ngozi kwa ajili ya wanafunzi mashuleni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama ongea na mwanao Steven Mengere almaarufu Stevenyerere ametoa shukrani kwa kiwanda cha uzalishaji wa viatu vya ngozi (SUMAJKT ) kwa kuona dhamira ya wazi kuungana nao na huku akisisitiza wasanii kuhakikisha inashirikiana na jamii inayowazunguka na kuwathamini kwani ni watu ambao wamekua wakinunua kazi za sanaa.

"Sifa ya Sanaa lazima uwe mbunifu na kutoka unarudisha katika jamii inayokuzunguka kuhakikisha unakua karibu na mashabiki zako katika kila hali".

Hata hivyo Steve ametoa wito kwa wadau ambao wangependa kuonyesha uzalendo wa kuunga mkono Kampeni hiyo kuhakikisha wananunua bidhaa za kinyumbani zaidi na kutembelea Kiwanda cha uzalishaji cha (SUMA JKT).

"Ilikua inaaminika kuwa Kiwanda hiki ni kwa ajili ya Wanajeshi pekee yao,La hasha.! ila kuna bidhaa ambazo mtu yoyote anaweza kutembelea na kupata kwa wakati hivyo tuunge mkono bidhaa za kinyumbani ili tuwe wazalendo, nimeshatoa taarifa kwa wadau wanaohitaji na ambao wangependa kutuunga mkono kununua bidhaa za viatu vya ngozi vyenye ubora zaidi na vinadumu muda mrefu."

Pia ameeleza kuwa Kampeni hiyo tayari imetembelea Shule za Mkoani Tabora, Kbiti na kwa sasa inatarajia kuwafikia wanafunzi katika Mkoa wa Mtwara na Lindi kwa wilaya 6 Vijijini.
Mkurugenzi Muendeshaji wa kiwanda cha viatu na bidhaa za ngozi SUMAJKT  Meja Mathias Peter John akimkabidhi viatu Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na mwanao Steven Mengere almaarufu Steve Nyerere mbele ya Waandishi wa habari leo Novemba 4,2022 makao makuu ya SUMAJKT jijini Dar es salaamu 












No comments: