MAADHIMISHO YA WIKI YA LISHE VIJIJINI YAFANYIKE – RC SENDIGA


Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ameelekeza halmashauri zote mkoani humo
kuandaa maadhimisho ya wiki ya utoaji elimu ya lishe bora katika ngazi za vijiji ili
kukabiliana na tatizo la udumavu.

Ametoa kauli hiyo leo (Novemba 04, 2022) mjini Sumbawanga wakati wa hafla ya
kukabidhi pikipiki Kumi na Mbili (12) kwa maafisa lishe wa halmashauri zilizotolewa na
serikali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la udumavu ambao kwa Rukwa upo asilimia
47.9 kwa takwimu za mwaka 2018.

Sendiga alibainisha kuwa maadhimisho hayo yakifanyika itakuwa jukwaa zuri la
wataalam wa lishe kutoa elimu ya uandaaji vyakula bora na ulaji sahihi kwa kutumia
vyakula vinavyopatikana kwenye mazingira ya Rukwa kwa kuwa mkoa huo ni mzalishaji
mkubwa wa mazao ya chakula.

Akitoa taarifa ya vifaa hivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Ibrahim Isaack
alisema jumla ya pikipiki Kumi na Mbili zimetolewa kwa Halmashauri za Kalambo (4),
Sumbawanga Vijijini (3), Nkasi (3) na Manispaa ya Sumbawanga (2).

Dkt. Ibrahim alisema pikipiki hizo zitakwenda kufanya kazi ya elimu ya lishe, kuboresha
utoaji chanjo na kufuatilia magonjwa ya milipuko vijijini.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (wa kwanza kushoto) akipata maelezo kuhusu pikipiki (12) zilizotolewa na serikali kwa ajili ya maafisa Lishe kwenye halmashauri za Rukwa leo mjini Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Queen Sendiga akikata utepe wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki (12) kwa maafisa lishe wa halmashauri za Rukwa zitakatumika kutoa elimu ya kudhibiti udumavu vijijini.
 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga kaiwasha moja kati ya pikipiki (12) alizozikabidhi leo kwa Maafisa Lishe wa Halmashauri za mkoa huo ili zikatumike kutoa elimu ya lishe bora na chanjo vijijini. Kushoto ni Afisa Lishe wa Manispaa ya Sumbawanga  Bw. Nassoro Chacharika aliyekabidhiwa pikipiki hiyo leo.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa) 

No comments: