MSAMA ASEMA KINANA NDIYE MGENI RASMI TAMASHA LA KUMUOMBEA RAIS SAMIA NA TAIFA JIJINI MWANZA


Kampuni mahiri inayoandaa matamasha ya Injili nchini ya Msama Promotion, imeandaa tamasha kubwa la kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan pamoja na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 15,2022 jijini Dar Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion,Alex Msama amesema tamasha hilo litakalosheheni Wasanii mbalimbali wa nyimbo za Injili linatarajiwa kufanyika Novemba 6, 2022 katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.

“Katika tamasha hilo litakalokuwa la aina yake litafanyika katika uwanja wa CCM Kirumba,na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM,Kanali Mstaafu Ndugu Abdulrahman Kinana’’amesema Msama.

Msama amesema tamasha hilo litaanzia jijini Mwanza na kutakuwepo na waimbaji mbali mbali mahiri wa nyimbo za injili kutoka ndani na nje ya Tanzania, akiwemo Rose Mhando, Christina Shusho, Boniface Mwaitege, Eveliny Wanjiru Kutoka Kenya naJoshua Ngoma Kutoka Rwanda.

“Nimewataja Waimbaji hao wachache tuu, lakini wako wengi na wanaendelea kuongezeka kutokana na mazungumzo yetu tuyaoendelea kuyafanya baina yetu na wao kuhakikisha tamasha hilo linafana vilivyo”,amefafanua Msama

Katika hatua nyingine Msama amesema Tamasha hilo ambalo litahusisha Waimbaji mbalimbali wa nyimbo za Injili wa Ndani na Nje ya Nchi, limelenga kuiweka Tanzania kwenye maombi pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan.

"Tunajua Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ni Mchapakazi na amejitoa kwa ajili ya Kuwatumikia Watanzania, kwa hiyo Dhamira ya Tamasha hili ni Kufanya Maombezi kwa ajili ya Kumuomba Mungu aweze kumfanyia wepesi Rais wetu kwenye Utekelezaji wa majukumu yake ya Kila Siku kwa ajili ya Watanzania" amesema Msama.

Msama amewaomba Watanzania wote kuungana pamoja katika siku hiyo kuliombea Taifa letu huku akiwasihi wakazi wa Mwanza na mikoa ya jirani kufika mapema tarehe 6 kushiriki na kushuhudia Burundani kutoka wa waambaji mashuhuri watakaokuwepo siku hiyo.

Kwa Upande wake Mratibu wa Tamasha hilo Emmanuel Mabisa amesema mpaka Sasa Maandalizi mbalimbali yamekamilika kwa Kuzungumza na Wachungaji pamoja na Maaskofu mbalimbali kushiriki Tamasha hilo la Maombezi kwa ajili ya Taifa.

"Tayari Wachungaji na Maaskofu mbalimbali wamethibitisha kushiriki kwenye Tamasha hilo kwa ajili ya Kupiga maombi kwa ajili ya Rais Wetu na Taifa kwa Ujumla kwa maana yatakuwa ni maombi ya Kitaifa" ameeleza Mabisa.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion,Alex Msama akizungumza na Waandishi wa habari leo Oktoba  15, 2022 kuhusu tamasha la Kumuombea Rais na Taifa litakalofanyika Novemba 6,2022  katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza. Pichani kusho ni mmoja wa Waratibu wa tamasha hilo Emmanuel Mabisa

No comments: